Jumanne, Septemba 17, 2019
Jumanne, Septemba 17, 2019,
Juma la 24 la Mwaka
1 Tim 3:1-13
Zab 101: 1-3, 5-6
Lk 7: 11-17.
Kazi mbalimbali za kufanya
Mawaidha ya Mt. Paulo kwa Timotheo yanaonesha picha ya namna mfumo wa uongozi ulivyokuwa. Hatusikii habari kuhusu mitume, manabii au waponyaji kama ilivyokuwa katika siku za Yesu bali tunasikia kuhusu majukumu ya maaskofu, mashemasi, wazee wa kanisa na wajane.
Kadiri kanisa lilivyoenea katika nchi za mediterania kulikuwa na matatizo katika uongozi na kanisa lilipata changamoto ya kuteswa kwa watumishi wake, hivyo kulikuwa na uhitaji wa kutengeneza mfumo mzuri wa uongozi. Kanisa lilitakiwa kubadilika kutokana na nyakati kutoka katika mfumo wa maisha ya mitume hadi mfumo mpya wa madaraja. Bado kanisa hili liliendelea kuwa moja na liliendelea kuwa mwili wa Kristo. Mt. Paulo anasema kuwa; Mwili ni mmoja lakini viungo ni vingi, viungo vyote yaani wanajumuiya wa kikristo ni mwili mmoja katika Kristo. Katika maelezo haya anamaanisha kuwa kuna aina mbalimbali za talanta na vipawa vinavyohitajika katika uhai wa kanisa.
Fadhila zote zilizotakiwa kwa maaskofu na mashemasi ni fadhila za kuigwa; askofu kuwa mtu asiyelaumika, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi na busara, mtu wa utarabibu, mkaribishaji, ajuaye kufundisha, si mtu wa kuzoea ulevi, si mpiga watu, mpole, si mtu wa kujadiliana, si mpendad fedha, mwenye kusimamia nyumba yake na mwenye kushika Imani na dhamiri safi.
Wasaidizi katika nyakati za shida
Katika nyakati za Yesu Wajane walikuwa watu waliokumbwa na matatizo ya kiuchumi pamoja na kijamii Zaidi ya watu wengine. Waliwategemea watoto wao kwa misaada kwasababu wame zao hawakuwepo tena. Hivyo mjane alifiwa na kijana wake alitesseka Zaidi ya wote. Katika injili ya leo tunasikia mjane mmoja akikutana na Yesu. Yesu alipomuona alimuonea huruma. Huruma hii ya Yesu inapelekea kurudisha uhai wa kijana wa mjane huyu. Jambo la kushangaza mwanamke yule hakuomba jambo lolote lakini Yesu alivutwa kwa kuona majonzi aliyokuwa nayo. Mwanamke huyu hakumlilia Yesu wala kumuomba, lakini Yesu alimsaidia baada ya kutambua hali yake ya masikitiko na majonzi.
Bwana huyuhuyu mfufuka anakuja kwetu katika halizetu za maisha hasa katika nyakati za shida na majonzi, bila kusubiri maombi yetu kwake. Huruma yake ni msaada wetu wakati wa mahangaiko yetu. Tusibebe shida zeu kwa kuwa Yesu yuko nasi. Yesu anateseka nasi, hii ndiyo maana halisi ya huruma. Bwana Yesu atuoneshaye huruma anataka sisi pia tuoneshe moyo huuhuu kwa wahitaji, kuwasaidia kubeba mizigo yao kama Yesu anavyobeba mizigo yetu.
Maoni
Ingia utoe maoni