Alhamisi, Septemba 05, 2019
Alhamisi, Septemba 5, 2019.
Juma la 22 la Mwaka wa Kanisa
Kumbukumbu ya Mt. Teresia wa Kolkota.
MASOMO YA MISA
Kol 1: 9-14;
Zab 98: 2-6;
Lk 5: 1-11
Sote tumeitwa kuwa watakatifu
Mt. Paulo anafundisha kuwa utakatifu unapatikana katika matendo ya kawaida kabisa ya kila siku. Mambo yanayohusu maisha yetu ya kila siku kama vile ajira, masomo, afya, chakula na maisha ya familia yanaweza kufanyika kwa ajili ya Mungu kwa shukrani kubwa. Kama alivyowataka wanafunzi wake katika sehemu mbalimbali, Mt. Paulo anatufundisha sisi pia kuwa; ‘tuishi maisha mema yanayompendeza Bwana’. Hii inaashiria kuwa sote tumeitwa kuwa watakatifu. Kila mbatizwa amepewa neema na Bwana kutenda kwa kumpendeza Mungu. Tunachohitaji ni ujasiri na ufahamu, ili tuweze kujua wapi pa kutweka nyavu zetu.
Siyo asili yetu kutozaa matunda daima.
Ndugu wapendwa, wengi wetu tunaweza kuwa tumeshindwa kwa njia moja au nyingine. Tunaweza kuwa tumeshindwa kutimiza malengo yetu tuliyojiwekea. Labda, ipango au biashara tulizofanya zimetuletea matokeo hasi na kutotunufaisha kabisa. Mara nyingi mambo kama haya husababisha kupotea kwa matumaini. Katika injili ya leo kuna jibu kuhusu nyakati kama hizi. Katika injili tunasikia malamiko ya Mt. Petro kwamba; ‘tumefanya kazi usiku kucha lakini hatukupata chochote’ na baadaye tunamsikia Petro akisema ‘ondoka kwangu Bwana, ‘kwa kuwa mimi ni mwenye Dhambi’.
Ndugu zaangu, kushindwa au kuanguka katika jambo Fulani sio mwisho wa kila kitu kwasababu, Yesu yu karibu yetu kutusaidia katika shida zetu. Katika injili Yesu alibadilisha maudhi ya kazi usiku ule kuwa kazi yenye kuzaa matunda. Yesu alifanya hivi kwa kuibariki kazi yao na kuwazawadia samaki wengi. Zaidi ya hayo Yesu aliahidi kuwa; baadaye Petro angekuja kufanya naye kazi, kwa kuwavua watu kuelekea katika ufalme wa Mungu. Yesu yuko nasi daima hata katika nyakati za kushindwa kufanikiwa. Bwana Yesu huleta uhai kutoka katika hasara au katika kushindwa kwetu. Ili neema ya Mungu ifanye kazi katika nyakati hizi tunatakiwa kuvumilia. Tunatakiwa kushusha nyavu zetu chini Zaidi kwa kutii neno la Mungu kama Petro na wenzake walivyofanya.
Maoni
Ingia utoe maoni