Jumanne. 26 Novemba. 2024

Tafakari

Jumapili, Septemba 01, 2019

Jumapili, Septemba, 1, 2019.
Dominika ya 22 ya Mwaka

Ybs 3:19-21, 30-31;
Zab 67: 4-7, 10-11;
Ebr 12: 18-19, 22-24;
Lk 14: 1, 7-14.


UNYENYEKEVU: TUNU TUPATAYO KWA UFALME WA MILELE

Katika Injili zote nne, Yesu anaoneshwa mtu anayependa kuwa na watu, na hata kuhudhuria matukio ya kijamii kama harusi, kualikwa kwenye chakula, nk. Alienda mpaka hata kwenye nyumba za watoza ushuru waliokuwa wanachukiwa na Wayahudi na pia katika nyumba za Mafarisayo ambao kila mara walimjaribu kwa mitego ya maswali na kumlaumu na ambao mwishoni walipanga hata kifo chake.

Katika Injili ya leo tunamuona Yusu alikuwa amealikwa kwa chakula katika nyumba ya kiongozi wa Mafarisyo na Yesu kama kawaida yake anakubali mwaliko. Injili inasema kwamba Mafarisayo walikuwa wanamuangalia kwa makini na kwa sababu ilikuwa ni Sabato inaonekana mlo huu ilikuwa ni kwa sababu ya kumtega kuona kama atavunja sheria za Sabato. Lakini Yesu pia anawaangalia wao pia. Na hapo Yesu anawapa mfano.

Sehemu ya kwanza ya mfano huu unakuja kwa sababu Yesu aligundua kwamba kati ya wageni wengi walioalikwa walikuwa wakitafuta nafasi za mbele za heshima. Kwa Wayahudi sehemu ya heshima ni kwa wale waliokaa upande wa kulia au kushoto karibu na meza aliokaa mgeni rasmi aliyealikwa au mwenye sherehe. Kwahiyo Yesu anatoa mfano wake akitumia mfano wa karamu ya harusi ambao ilikuwa ni tukio la kawaida katika jamii hii. Mafarisayo wakiwa ni watu wanaoheshiwa sana na Wayahudi kawaida walitegemea kukaa sehemu za heshima. Kwahiyo Yesu anawaonya akiwambia wasitafute sehemu za heshima kwasababu katika Ufalme wa Mungu haitakuwa hivyo. Mafarisayo walijua na kuamini kwamba kawaida wao wangekuwa wa kwanza kutumikiwa lakini hapa Yesu anafunga matumaini yao. Yesu anatambulisha kitu kidogo sana na chenye thamani sana “unyenyekevu” kadiri unavyokuwa mnyenyekevu kadiri unavyoheshimiwa.

Mafarisayo somo hili lilikuwa ngumu kwao. Sisi nasi wakati mwingine tumejikuta tukitafuta heshima. Kumbuka maneno ya Yesu “watakao jikweza watashushwa na watakao jishusha watakwezwa”. Tubadilike leo tuache hali yetu yakutafuta heshima ya muda tuu na tutafute heshima ya uzima wa milele ambayo inapatikana kwa unyenyekevu.

Katika sehemu ya pili ya mfano Yesu naongea na aliyemualika kuhusu wale walioalikwa. Yesu hapa anasema kitu ambacho ni jambo la kufikirika kwa akili zetu kwamba, kama mtu akimualika rafiki, ndugu, waheshimiwa, anatagemea kupata kitu kwao tena. Kama mtu akitupatia zawadi katika sikukuu ya kuzaliwa anategemea yeye naye akiwa na siku yake ya kuzaliwa nawe utampelekea chochote. Katika hali nyingine, Yesu anatualika tuwaalike masikini, vilema, wasiojiweza nk, ili tusitegemee kitu kutoka kwao kama malipo. Yesu anatu hakikishia kwamba kitendo hicho hakitaenda bure bila malipo kwa hakika utalipwa mbinguni. Tunachopata hapa ni kwamba tukifanya jambo ili kutegemea heshima na kusifiwa ni kwamba tunakuwa tumepoteza tuzo letu huko mbinguni badala yake tufanye yote kwa unyenyekevu kwa waliowanyonge katika jamii, tutapokea tuzo letu huko mbinguni.

Katika maisha yetu ya kila siku kawaida kuna vita kati ya maringo na unyenyekevu. Tukiacha maringo yetu yakikuwa tutaanza kutafuta heshima na kama tutaacha unye nyekevu ukue tutaanza kuwa wadogo na wenye upole na upendo kwa wote. Yesu leo ametushauri leo tuwe wanyenyekevu, ni juu yetu kukubali au kukataa na kuendeleea kuwa kama mafariso ambao waliendela mpaka kumua Yesu.

Sala:
Bwana, nifanye mpole na mnyenyekevu wa moyo kama wewe.
Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni