Jumapili, Agosti 18, 2019
Jumapili Agosti, 18, 2019
Juma la 20 la Mwaka c wa Kanisa
Yer: 38:4-6.8-10
Ebr.12:1-4
Lk 12: 49-53
MUNGU NI MOTO UNAOPENDEZESHA VYOTE.
Katika soma la kwanza tumeona nabii Yeremia alitumwa na Mungu kuwaeleza wayahudi kwamba mji Yerusalemu utatekwa na jeshi la mfalme wa Bebeli. Lakini wakuu wa Yuda walichukizwa na ukweli huo wakaamua Yeremia auawe. Kutupwa Yeremia katika matope na kuokolewa kwake kunatazamwa na wakristo kama mfano wa kifo na ufufuko wa Yesu.
Soma la pili mtume Paulo anatuamibia waraka huu uantusimulia namna watakatifu walivyovumilia taabu na kupata tuzo lao; pia namna Yesu alivyostahimili mateso na kupata utukufu. Uvumilivu wa watakatifu hao na hasa wa Bwana Yesu ni mfano wa hizimo katikakuzichukua taabu zetu za kila siku tukitaka kuufikia utukufu huo.
Katika Somo la Injili Yesu anatupa tahadhari nyingine kwamba kwa ujio wake yaweza kuwa amekuja kuwasha moto duniani. Na hili kweli linatokea nyakati zetu, tumeshuhudia familia zikitengana kwa kigezo cha Injili tena wote wakiwa wafuasi wa Kristo. Wengine hujidai wanamuelewa Kristo zaidi na kuwadharau wengine. Wengine huamka hata usiku wa manane na kuwasumbua wengine kwa sala za kelele kwa kisingizio wanafukuza pepo na kuwafanya wengine wasilale. Wengine hujifanya wafafanuzi wazuri wa maandiko zaidi kuliko wengine na hivyo kuishia kushindana. Yesu haya aliyatambua yatakuwepo. Paulo anatupatia jibu zuri sana katika (Ef 3:14-21), hamna namna nyingine ya kuonesha kwamba sisi ni wafuasi wa Kristo isipokuwa kwa njia ya upendo. Utengano sio sifa ya Kristo.
Yesu aliwashtuwa wafuasi wake pale aliposema kuwa amekuja kutupa moto na kusababisha mgawanyiko badala ya amani duniani. Je, ni aina gani ya moto ambao Yesu alikuwanao akilini mwake? Moto katika neno la Kibiblia ulihusianishwa na Mungu pamoja na kuhusianishwa na matendo yake ulimwenguni katika maisha ya watu wake.
Wakati mwingine Mungu anadhihirisha uwepo wake kwa uwepo wa moto, kama vile kichaka kiwakacho ambacho hakiteketei alipoongea na Musa (Kut 3:2). Alama ya moto ilitumika pia kuwakilisha utukufu wa Mungu (Eze 1:4, 13), uwepo wa ulinzi wake (2Fal 6:17), utakatifu wake (Kum 4:24), hukumu ya haki (Zek 13:9), na hasira yake dhidi ya dhambi (Isa 66:15-16). Pia imetumika pia ikimaanisha Roho Mtakatifu (Mt 3:11 na Mat 2:3). Moto wa Mungu unasafisha na huondoa uchafu, na unavuvia mwanga na hofu ya kumuabudu Mungu na nguvu ya neno lake ndani yetu.
Basi tuchukue mfano mmoja kutoka kwenye Biblia uhusuo moto – kichaka kiwakacho katika kitabu cha Kutoka. Kichaka chaonekana kuwa kinawaka tu badala ya kuteketea. Sifa ya asili ya moto ni kuchoma na kuteketeza. Lakini kinachotokea hapa ni hali ya tofauti. Je, unasema nini juu ya Mungu wetu? Ndio Mungu wetu ni moto, sio moto uharibuo bali moto unaobadilisha. Unatuunguza sisi kufikia uzuri. Mara utakapo unguzwa na moto huu katika uhalisia unakuwa kiumbe kipya, unatoka kwenye uovu na kusimama njee. Kama upo katika familia yako ya watu wanne na ukawa umeunguzwa mpaka kufikia uzuri katika uhalisia utakuwa nje. Unasimama njee ukiwa tofauti na hapo huenda ukachukiwa au kupendwa au kuigwa. Inawezekana familiya yetu na marafiki zetu kuwa maadui zetu. Kama mawazo yao yatatuzuia sisi kutenda yale tunayoyajua kuwa Mungu anapenda sisi kuyafanya ni dhahiri tutamtii Mungu zaidi kuliko wao, na hapo huenda uadui ukawepo. Je, upendo wa Yesu Kristo unakusukuma wewe kumuweka Mungu kwanza kwa yale yote uyatendayo (2 Kor 5:14)?
Tusitumie pia sala kama kisingizio cha kuwakashifu wale wasio sali. Tusijione wema zaidi kwasababu tu sisi tunaenda kanisani na wengine hawaendi. Badala yake sisi tuwaombee waregevu na kuwashauri kwa upendo na upole ili waweze kuvutwa nao kumtumikia Kristo. Tusiwashe moto duniani wa fujo kwakutumia Injili ya Kristo.
Sala:
Bwana, naomba upendo wako unitawale na uyarekebishe maisha yangu.
Amina
Maoni
Ingia utoe maoni