Ijumaa, Julai 26, 2019
Ijumaa, 26 Julai, 2019,
Juma la 16 la Mwaka
Kumbukumbu ya Watakatifu Yoakim na Anna,
Wazazi wa Bikira Maria
Ybs 44: 1, 10-15;
Zab 132: 11, 13-14, 17-18;
Mt 13: 16-17
KUITWA ILI KUMSIKILIZA NA KUMUONA MUNGU!
Yoakim (maana yake Mungu anaandaa) na Anna ( maana yake Neema) ni wazazi wa Bikira Maria. Mapokeo yanasema waliishi Galilaya kwanza na baadae wakaishi Yerusalemu ambapo Bikira Maria alizaliwa na kukua hapo. Tunajua kidogo sana kuhusu maisha ya Watakatifu Yoakimu na Anna, lakini tunatambua kwamba ni lazima walikuwa watu wenye maadili mema sana mpaka kuweza kumlea Bikira Maria mama wa Mungu.
Leo katika kuwakumbuka Babu na Bibi wa Bwana wetu Yesu Kristo, tunaitwa tuwaheshimu pia wazee walio na umri mkubwa. Katika somo la kwanza kutoka katika kitabu cha Yoshua Bin Sira, tunaalikwa tuwahesimu wazee wetu. Anaye heshimu wazee na wazazi anatii mapenzi ya Mungu.
Katika somo la Injili Yesu anawasifu wasikilizaji wake kwasababu Masikio yao yamesikia na macho yao yameona. Anawaambia wana heri. Macho ni kwaajili ya kuona na masikio ni kwaajili ya kusikia. Mara nyingi tunashindwa kuona na kusikia. Katika hali ya nnje tunaweza kuwa tunasikia na kuona. Lakini Yesu anapoongelea kuhusu kuona na kusikia, inamaana pia ya ndani. Ni zaidi ya kusikia na kuona katika hali ya kawaida. Inamaana kwamba mmoja anaweza kuona Mungu akifanya kazi ndani yake na ndani ya wengine. Mara nyingi Mungu anafanya kazi katika matukio yetu mbali mbali ya maisha. Katika hali hizo tunashindwa kuona mkono wa Mungu nakumsikiliza anapoongea na sisi. Tunaweza kusikiliza ulimwengu mzima ukiongea na sisi, lakini tukishindwa kumsikiliza Mungu yote yanakuwa bure. Katika hali hiyo hiyo, tunaweza kuuona Ulimwengu mzima, lakini tukishindwa kumuona Mungu, yote yanakuwa bure.
Wakati Yesu akihubiri, baadhi walimsikiliza wakaona ufalme wa Mungu ukija kati yao. Mungu siku zote anaongea nasi, anatupa nafasi ya kumuona yeye kwa njia mbali mbali. Tukisoma neno la Mungu, Mungu anaongea nasi. Hatumuoni Mungu uso kwa uso, tunamuona yeye katika Maskini, katika Ekaristi Takatifu juu ya Altare, katika watu waliowekwa wakfu, katika Jumuiya ya watu waliojikusanya kwa Jina lake na kwa wenzetu. Tukichukua mfano wa Yoakimu na Anna na zaidi sana mfano wa Bikira Maria mwana wao, tunaitwa leo kumuona Mungu na kumsikiliza.
Sala:
Baba Mungu nisaidie mimi nilikusikilize na kukuona ili niweze kufanya mapenzi yako kila wakati.
Amina.
Maoni
Ingia utoe maoni