Jumanne. 26 Novemba. 2024

Tafakari

Jumamosi, Julai 06, 2019

Jumamosi, Julai 6, 2019.
Juma la 13 la Mwaka

Kumbukumbu ya Bikira Maria ya Jumamosi

Mwa 27: 1-5, 15-29;
Zab 135: 1-6;
Mt 9: 14-17


YESU BWANA HARUSI WETU MPENDWA!
Dira ni kifaa kinachotumika na watu kama wanajeshi, nahodha nk. Masomo ya leo ni kama dira, yana tufunulia Umungu wa kweli ndani ya Yesu. Kama dira inavyo muongoza nahodha ili kufika mwisho wa safari yake. Pia Yesu ni dira yetu anatuongoza ili tufike kwenye furaha ya milele. Lakini furaha hii haipatikani hivi hivi, ni lazima kupitia mawimbi mbali mbali kama nahodha anapopitia njia mbali mbali na sehemu asiyo ifahamu ili kufikia lengo lake. Yesu ni nahodha pekee aliyekuwa na hakika ya ushindi wake, mateso, kifo na ufufuko. Hata njia yetu itakuwa hivyo hivyo. Pili maisha yetu ni kama kioo kinacho tuonesha jinsi tulivyo. Lakini tunapomchukua Yesu, kama divai mpya na mawazo mapya na mtazamo mpya wa ukweli, yeye anakuwa kioo chetu cha kumulika maisha yetu nakutambua ukweli halisi ya kuwa tunapaswa kuwa tofauti zaidi na jinsi tulivyo sasa. Maisha ya zamani tuliyo jijengea yenye sheria ngumu na tena nyingine zenye ubinafsi na chovu au mambo mengine yanayopingana na upendo wa Yesu yanapaswa yaondolewe na kuwa kiumbe kipya na kuweka mambo mapya yaliosimikwa katika upendo wa Yesu.

Kwa hiyo kuna ulazima wa kubadili maisha yetu. Kwakumweka Yesu kama kioo mbele yetu ili amulike maisha yetu. Hapo tutaona nafsi yetu ilivyo tofauti na nafsi ya Yesu ambaye sisi wote tumeitwa kuishi maisha yake. Maisha yangu yanapaswa yawe kama maisha ya Yesu, kama nashindwa kuishi kama Yesu alivyo basi napaswa kubadili mienendo yangu. Tutafute ukweli kuhusu nafsi zetu zaidi na tuondoe ile hali yakutaka kujua tuu ukweli kuhusu maisha ya wengine na kuficha yetu. Tunapoteza muda mno kutaka kujua nafsi za wengine, tuanze na nafsi zetu na moja kwa moja mafanikio yataonekana na wengine. Tuombee neema ya Mungu ituongoze ili tuweze kubadili maisha yetu kwanza katika kweli ya Yesu kabla hatuja thubutu kuwarekebisha wengine.

Kwa upande mwingine, tunaitwa kuwa huru. Tumeitwa kuwa huru na kufurahai maisha katika hali kamili na kufurahi furaha kamili anazo toa Mungu ili tuzifurahie kama Mungu anavyo penda. Uhuru ulio wa kweli kabisa ni ile hali ya kuwa na Bwana harusi kati yetu. Ni furaha ya harusi ya mwana-kondoo. Tumeitwa kusherekea umoja wetu na yeye milele. Kwa hiyo wageni hawawezi kuomboleza wakati wapo na Bwana harusi kati yao. Lakini siku zinakuja ambapo Bwana harusi ataondolewa kati yao, ndipo wakatapo funga.

Kuna muda katika maisha yetu ambapo Bwana harusi anachukuliwa. Muda huu unaweza kuwa muda ule tunao hisi kumkosa Kristo katika maisha yetu. Hili linaweza kuja kwasababu ya matokeo ya dhambi zetu, lakini pia inaweza kuja kwasababu ya sisi kuwa karibu na Kristo. Kufunga inaweza kutusaidia sana kuepuka na mambo mengi tulio jifunga nayo katika maisha yetu. Imejaa hali ya kutusaidia kuongoza matamanio yetu na kutakasa tamaa zetu. Kufunga ni sehemu ya kuzamisha imani kutusaidia kukutana na Bwana Harusi. Kufunga inaweza kuchukua hali mbali mbali, lakini moyoni ni kitendo cha kujikatalia na kusogea karibu zaidi na Mungu. Inatusaidia kuepukana na tamaa zetu za kidunia na kutuvuta karibu zaidi na Kristo.

Tafakari ni mara ngapi unatamani kuzama katika maisha ya Kristo. Je, unatamani kukutana na furaha ya Yesu? Je, unatamani kumuiga yeye? Kama unapenda kuhisi furaha ya Bwana harusi, Yesu, kabidhi kila kitu kwake katika sala. Na hapo endelea kumtolea hali zote za kufunga, na kujikatalia. Endelea kutolea sadaka kwa Mungu na utaona matunda yake.

Sala:
Bwana, natamani kuwa nawe katika maisha yangu zaidi ya chochote. Nisaidie kuona vile vitu vinavyo endana na upendo wako na unitakase ili moyo wangu uweze kuishi katika uhuru na furaha unayopenda mimi niishi. Yesu nakuamini wewe.
Amina

Maoni


Ingia utoe maoni