Ijumaa, Julai 05, 2019
Ijumaa, Julai 5, 2019,
Juma la 13 la Mwaka
Mwa 23:1-4,19, 24:1-8,62-67;
Zab 105: 1-5;
Mt 9: 9-13
MDHAMBI ANAKARIBISHWA KWA HURUMA
Embu jaribu kufikiri mtu anakuwa daktari asiyependa kuona au kushughulika na wagonjwa, yeye anapenda tu watu wenye afya njema. Nadhani atakosa kabisa wakutibu kwasababu watu wenye afya njema hawahitaji kutibiwa. Huu ndio msemo anaotumia Yesu katika Injili baada ya kulaumiwa kuwa rafiki wa wenye dhambi. Ingekuwa ni ajabu kabisa kwa yeye kuja ulimwenguni kama asingekuja kumpatanisha mwanadamu mkosefu na Mungu Baba yake. Tunajua nikwa jinsi ghani alivyofanikiwa katika hili, ambapo Mathayo aliyekuwa mdhambi sio tuu anabadilika bali anakuwa pia mtume wa kazi yake. Ni kitu ghani kilichopo ndani ya Kristo kinachowavutia wenye dhambi kwenda kwake? Ni kwasababu ya upendo aliokuwa nao na huruma. Pale ambapo Mafarisayo walikimbilia ili kwenda kuhukumu, Yesu aliangalia uzuri uliopo ndani ya mtu na watu walimwitikia kwa jinsi yake yakuwaita kwa upendo. Yesu hakuja kwa ajili ya wale wanaojiona wenye haki, bali alikuja kuwaita wakosefu kutoka katika utumwa wa dhambi na kuwaleta katika uhuru wa watoto wa Mungu, naye alifanya hivyo kwakuwa kati yao.
Sisi nasi tunaalikwa kuwa na huruma kwa ndugu zetu na watu wote wanaliotukosea. Pia kama wajumbe wa neno la Mungu tusijione kwamba sisi tunastahili zaidi kuliko wengine, vyeo vyetu tujue ni jukumu tulilopewa la kuwa watumishi, kuwatumikia wote bila kuwatenga wengine. Baba Mtakatifu Fransisko alisema “Mchungaji anapaswa kunukia harufu za kondoo wake” wale waliopewa jukumu la kuwachunga kondoo wa Mungu, tunaitwa kuwa watumishi waaminifu, wenye kupata muda wa kuongea na kondoo wetu na kuwatumikia, usiwe juu sana kiasi cha kondoo kushindwa kukufuata na kutaka ushauri kwako. Kuwa mchungaji sio kuwa “Boss” badala yake ni kuwa mtumishi wa watumishi wa Mungu. Katika kitabu cha Malaki 2:5..kuwa kuhani/Padre/mjumbe wa Mungu nikutambua “kwa midomo yako utawapa watu akili na matashi mema na watu watataka ushauri na maelekezo kutoka kwako kwakuwa wewe ni mjumbe wa Mungu….”.
Kwa wale waliochaguliwa viongozi wa jumuiya au uongozi wowote ni lazima kutambua kuwa kwakuwa hivyo sio kuwa Mkristo zaidi ya wengine bali ni utumishi wa watumishi wa Mungu. Tuombe neema yakutumia uongozi tuliopewa na Mungu ili kuwaongoza wote bila kuwapenda matajiri tuu na kuwaacha maskini au kuwapenda wanaosali na kuwachukia wasio Sali. Badala yake tutumie njia njema ya kuwaonesha upendo na huruma kama Yesu, wanaweza kurudi na kuwa wema tena. Sisi zote kwa maisha yetu tumlete Kristo aonekane kwa watu.
Sala:
Bwana, ninarudi kwako katika mahitaji yangu kwako ninakiri dhambi zangu. Ninakuomba unisamehe kwa kukukosea wewe na ninatambua kuwa ni wewe tu jibu pekee kuhusu dhambi zangu. Naomba Bwana uwe na huruma kwangu na unisamehe dhambi zangu zote.
Amina
Maoni
Ingia utoe maoni