Jumanne. 26 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatatu, Julai 01, 2019

Jumatatu, Julai, 1, 2019,
Juma la 13 la Mwaka wa Kanisa

Mwa 18:16-33
Zab 49: 16-23;
Mt 8: 18-22


MFUASI, HAPA NA SASA!
Yesu ni uwepo wa Mungu katika maisha yetu. Maisha yetu ya Ukristu ni kuishi maisha ya Yesu. Sio tuu ujumbe wake bali kuishi kama Kristo alivyoishi. Imani ya Kikristo sio “Dini ya neno la Mungu tu” wala sio ya “maneno yalioandikwa na kufunikwa bali ni maneno ya kuyaweka ndani yetu na kuyaishi” (Papa Mstaafu Benedict xvi).

Leo, tunaweza kupata picha ya kwamba Yesu anahitaji kitu ambacho hakifikiri kwa wale wanaotaka kumfuata. Kwa yule mfuasi aliyetaka kwenda kumzika Baba yake, Yesu akamwambia “nifuate na waache wafu wazike wafu wao”. Sentensi hii haimaanishi kwamba Yesu ni mtu aisiye na huruma, bali Yesu anataka kutuambia kwamba sisi hatupaswi kusubiri kwanza tuweke mambo yetu vizuri ndio tumfuate yeye. Sisi pia wakati tunaitika wito wa Mungu, tunakuwa na mawazo, nataka nitimize malengo yangu kwanza kuhusu familia yangu na mipango yangu yote kabla sijaanza kumfuata Bwana. Leo tunaitwa tutambue ujumbe huu kwanza kwamba, Mungu ndiye anayekuja kwanza na mengine yote yatafuata. Ufuasi wa Kristo unaanza sasa hivi ninavyosoma asali itokayo mwambani (sasa hivi muda huu huu). Kama nikuazimia kuacha dhambi ni sasa hivi hivi sio baadaye, itika wito wa Yesu sasa hivi na anza maisha mapya.

Sala:
Bwana, nisaidie mimi niweze kutambua kwamba wewe mwenyewe unauwezo wa kutawala yote, nisaidie mimi nikabidhi yote kwako yanayonisonga nishindwe kuitikia wito wako vizuri.
Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni