Jumanne. 26 Novemba. 2024

Tafakari

Jumamosi, Juni 22, 2019

Jumamosi, Juni, 22, 2019,
Juma la 11 la Mwaka wa Kanisa

2 kor 12:1-10
Zab 88: 4-5, 29-34;
Mt 6: 24-34

BWANA WANGU NINANI- MUNGU AU PESA?

“Moyo uliogawanyika ni moyo wa huzuni.” Wote tunajua hili kwasababu ni moyo ulio na wasi wasi na usiojiweza. Leo tunasikia Yesu akituambia hatuwezi kutumikia mabwana wawili. Hatuwezi kujitoa kwa Mungu moja kwa moja kama tumetekwa na pesa. Kwanini? Kwasababu vyote vinahitaji kujikita na kujitoa. Mungu anahitaji majitoleo ya kweli si kwaajili yake bali kwaajili yetu wenyewe. Hatuwezi kuwa na furaha kabisa au furaha ya kweli bila Mungu. Na ni Mungu mwenyewe anaweza kurudhisha tamaa ya moyo wa Mwanadamu.
Hakuna mtu anaeweza kuwatumikia mabwana wawili kwa muda mrefu. Kwasababu wakati Mabwana wote wawili wakiwa wanatembea pamoja, anaweza kuwafuata nyuma yao lakini watakapo amua mmoja kwenda uelekeo wake na huyu wake, lazima achague ni yupi wakumfuata. Haijalishi ni mara ngapi watu wamemuasi Mungu na kufuata au kuabudu mali na pesa, Mungu haachi kamwe kuwapigania warudi kwake. Tujikumbushe maneno haya ya Mungu “Sitawaacha kamwe wala kuwakataa ninyi” (Kumb 31: 6). Somo la kweli katika historia ya Mwanadamu ni kwamba-Hakuna mtu anayeweza kuwatumikia mabwana wawili katika hali ya kweli. Mkristo kwa kweli hawezi kutenda haki ya Mungu kwakujiingiza kabisa katika mali na anasa za ulimwengu huu.
Uovu wa kujaribu kugawanya uaminifu wetu unajikita katika kushindwa kwetu kutumainia Upendo wa Mungu Baba yetu. Tunajaribu kutafuta ulinzi wa maisha yetu katika mali na utajiri wetu. Tunafanya kila liwezekanalo kulinda heshima yetu katika mali, tunadhani tukipungukiwa tutadharauliwa na watu, kwahiyo siku zote tunajaribu kujilinda kuweka mambo yetu vizuri bila kujali kama na muumiza mwanadamu mwenzangu. Tunawatumikisha wengine wanateseka bila maji au chakula, ali mradi nimepata faida na utajiri wangu ubaki pale pale. Tunaogopa kuwasaidia wengine kwasababu tunadhani tutapungukiwa. Roho na akili yetu haina Amani usiku kucha kwasababu natafuta jinsi ya kutegemeza utajiri wangu, tumekamatwa sana na mali mpaka tunasahau nafsi ya Mungu katika maisha yetu. Tunakimbilia kwenye biashara kiasi chakushindwa hata kufanya ishara ya msalaba ili Mungu abariki mipango yetu. Mungu ni namba moja, mengine yote ni sifuri, tujitahidi kuitanguliza hii numba moja ili hizi sifuri zinazofuata nyuma yake zifanye yote yawe mengi, lakini ukitanguliza sifuri badala ya moja nadhani unajua utapata nini.
Kwa ufupi maisha yetu yatawaliwe na Mungu, chochote kamwe kisichukue nafasi ya Mungu. Mungu anapenda maadili yetu na thamani ya yote tulionayo yajengwe katika msingi wake yeye mwenyewe na hapo yataleta furaha na Amani kwetu. Mungu anajua mahitaji yetu hata kabla hatuja mwomba na anawapa wote kwa upendo wanao mtumainia.

Sala:
Bwana naomba usinifanye maskini wala usinifanye tajiri mno, nishibishe kwa chakula ninacho hitaji nisije nikashiba mno nikakutukana nikasema “Mungu ni nani kwani?” au nisiwe maskini mno nikaiba nikalikashifu jina lako Mungu.
Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni