Jumatano, Juni 05, 2019
Jumatano, Juni, 5, 2019,
Juma la 7 la Pasaka
Mdo 20: 28-38;
Zab 68: 33-36 (R. 33);
Yn 17: 11-19.
THAMANI YA SALA YA YESU!
“Baba Mtakatifu, uwakinge kwa jina lako takatifu” (Yn 17: 11). Kukingwa huku kulifanywa na Bwana wakati akiwa na wafuasi wake, lakini sasa anarudi kwa Baba. Yesu ameshaongea na wafuasi wake tayari juu ya hatari itakayo wakumba kutokana na Imani yao. Kwahiyo, anawaombea wale wote watakaomfuata kizazi baada ya kizazi. Anawaombea wafuasi wake ili waweze kufunikwa na kukingwa kwa jina la Baba. Hawaombei ili wawe matajiri na maarufu ulimwenguni, hawaombei wasipatwe na changamoto, magumu, majaribu, vishawishi na mateso. Anaomba ili sote tuwe wamoja, kwakutawala hisia zetu binafsi na vionjo binafsi. Kukingwa kwa wafuasi inahusisha kuwapa furaha hata wakiwa katikati ya kuchukiwa na kukataliwa na Ulimwengu.
Hawakuwa wa ulimwengu, kama vile mkombozi asivyokuwa wa ulimwengu. Kwahiyo, ulimwengu utawachukia na kuwapinga. Sala ya Bwana wetu, haituambii kwamba shetani hatatutafuta nakujaribu kututeka, bali inatuhakikishia kwamba tutalindwa wakati tutakapo jaribiwa na muovu. Kulindwa na Baba inabeba furaha na kuwa imara katika mapingamizi haya. Mwisho kabisa anaomba kwaajili ya wokovu wetu. Bwana wetu hakuwa mkombozi wa kwakujitenga, bali katika kujitoa na kutii mapenzi ya Baba yake. Mwisho kabisa, majitoleo yake yalimpeleka mpaka juu ya msalaba kutukomboa. Tunatakatifuzwa kwa kazi ya Kristo Msalabani. Thamani aliyotoa pale msalabani kwaajili ya ukombozi wa mwanadamu, hamna binadamu yeyote angeweza kuitoa. Ilitolewa mara moja tu, na haiitaji kuitolea tena. Lakini pia kuna wakati sala zetu zina thamani. Kila sala aliyotolea Yesu kwaajili yetu ilihitaji sadaka yake pale msalabani. Tuombe Mungu ili sala zetu ziwe na thamani mbele ya Mungu, tukiongozwa na Roho Mtakatifu sala zetu zitakuwa na thamani mbele ya Mungu.
Sala:
Bwana, tukinge na mitego ya yule muovu.
Amina.
Maoni
Ingia utoe maoni