UTANGULIZI
Jumatano ya majivu ni mwanzo wa kipindi cha kwaresima katika kanisa. Ni ishara ya kuanza kwa siku arobaini za kutafakari kwa undani fumbo kuu la upendo wa Mungu linalofunuliwa kwa kujitoa kwake na kufa msalabani, kifo cha aibu ili kuichukua aibu yetu. Mama kanisa anatupatia kipindi hiki ili tuweze kutafakari njia na mienendo yetu.
KWA NINI TUNAPAKWA MAJIVU?
Majivu ni ishara ya majuto, nayo hufanywa kisakramenti kwa kubarikiwa na kanisa. Tunapopakwa majivu katika paji la uso hutusaidia kutafakari na kutukumbusha kuwa wanadamu sisi tu mavumbi na mavumbini tutarudi. Hutukumbusha zaidi kuwa maisha ya hapa duniani tunapita na safari yetu itakamilika pale tutakapoungana na Bwana na mwokozi wetu katika ufalme wako.
Angalia; Isaya 61:3, Ester 4:1-3, Yeremia 6:26, Ezekieli 27:30, Mathayo 11:21 na Luka 10:13
KWA NINI MAJIVU YAPAKWE KATIKA PAJI LA USO NA SI PENGINEPO?
Ishara yoyote iwekwayo katika paji la uso huonesha umiliki (soma Ufunuo 7:3, Ufunuo 9:4, Ufunuo 14:1, Ezekieli 9:4-6, ). Tunapochorwa ishara ya msalaba katika paji la uso ni ishara kwamba sisi tupo chini yake yeye aliyekufa msalabani kwa ajili yetu.
Hali kadhalika hutukumbusha ishara ya msalaba tuliyochorwa na mafuta matakatifu siku ya ubatizo wetu, hutukumbusha ahadi tuliyoiweka siku hiyo ya ubatizo na kutuita tuishi maisha ya utakatifu
MANENO ANAYOTAMKA PADRE YANA MAANA GANI?
Tunapopakwa majivu Padre husema; Mwanadamu kumbuka u mavumbi na mavumbini utarudi AU Tubuni na kuiamini Injili.
Maneno haya kwa upande mmoja hutukumbusha tunapoelekea, tusisikitike kwamba siku moja tutarudi mavumbini bali tuwe na furaha kwani wakati miili yetu unarudi mavumbini roho zetu zitakwenda kuungana na Mungu Baba mbinguni.
Hivyo maandalizi tunayoalikwa kuyafanaya si maandalizi ya kuelekea mavumbini bali maandalizi ya kuelekeza roho zetu mbinguni. Ndio maana pia twaambiwa tubuni na kuiamini Injili.
MAJIVU HUTOKA WAPI?
Majivu tunayopakwa hutoka katika matawi yaliyotumika katika jumapili ya matawi ya mwaka jana. Majivu haya hubarikiwa na kuwa visakramenti. Hivyo majivu yanapoashiria toba na majuto pia hutukumbusha wema wa Mungu na utayari wake wa kutusamehe.
KWA NINI TUNATUMIA MATAWI YA JUMAPILI YA MATAWI?
Matawi haya yalimkaribisha Yesu Yerusalemu akiwa tayari kufa kwa ajili ya dhambi zetu, yalimpokea mfalme kwa furaha na shangwe kuu. Matawi haya yanapochomwa na sisi kupakwa majivu yetu yanatukumbusha kuwa ni kwa ajili ya dhambi zetu Mungu alimtoa mwanae wa pekee kufa msalabani kwa ajili ya dhambi zetu sisi wanaadamu. Hivyo hututafakarisha kuacha dhambi.
KANISA LIMEKATAZA NINI SIKU YA JUMATANO YA MAJIVU?
Tumekatazwa kula chakula siku ya Jumatano ya Majivu na kula nyama siku ya Ijumaa Kuu katika Amri ya Pili ya Kanisa.
NANI ANALAZIMA KUFUNGA SIKU YA JUMATANO YA MAJIVU NA KWARESMA?
Kila Mkristo aliyetimiza miaka 14 na zaidi anapaswa kufunga kula nyama (Ijumaa kuu) na mwenye miaka zaidi ya 21 kufunga chakula Jumatano ya Majivu
TUNAPOSEMA KUJINYIMA WAKATI WA KWARESMA TUNAMAANA GANI?
Kujinyima ni kujikatalia kitu ukipendacho mfano nyama, pombe, sigara, muziki, safari, maongezi n.k.
MWISHO
Wakati wa Kwaresma Waamini wanapaswa kujitakasa zaidi kwa kusali, kufunga, toba na matendo mema
Kipindi cha Kwaresima ni fursa makini ya kumkimbilia Mwenyezi Mungu, kwani kwa njia ya dhambi wamejikuta wakiwa mbali na Uso wa huruma ya Mungu, kiasi hata cha kupoteza imani na matumaini kwa Mwenyezi Mungu. Hii ni changamoto ya kumpenda Mungu na jirani badala ya kukumbatia malimwengu yanayoendelea kuwatumbukiza katika utupu wa maisha ya kiroho. Kwaresima ni kipindi cha waamini kukimbilia na kuambata huruma ya Mungu inayoganga na kuponya dhambi. Ni wakati wa sala, upendo na kufunga.
Maoni
Ingia utoe maoni