Ijumaa. 26 Aprili. 2024
feature-top

Makala hii ni sehemu ya Kitabu cha Kalamu kwa Vijana ambacho kipo katika hatua za mwisho kuchapishwa. Haki zote za mwandishi zimehifadhiwa.

Utangulizi
Kati ya mambo ambayo binadamu tunayaogopa sana mojawapo ni kifo, mwanadamu anaogopa kifo kwa kuwa kwanza kinamtenga na familia yake, ndugu, jamaa marafiki ambao amezoeana nao, pili anaogopa kifo kwa kuwa hafahamu ni wapi anapoelekea, jambo lingine linalowaogopesha watu juu ya kifo ni kuyaacha mambo ya dunia na raha zake ambazo amekua akizihangaikia kwa muda mrefu sana, kifo huogopwa pia kutokana na hukumu kwa wale wanaoamini uwepo wa Mungu na hukumu yake. Mwanadamu anapofariki huku nyuma huacha majonzi na simanzi kubwa haswa kwa wale waliokua wanamtegemea na wote ambao kwa namna moja au nyengine walikua wanafaidika na uwepo wake hapa duniani.
Kifo cha kijana mara nyingi huwa ni pigo zaidi, maana ujana ni wakati wa mtu kuchanua na jamii huwa imejiandaa sana kuvuna kutoka kwa vijana, anapofariki kijana jamii huhuzunika zaidi haswa kijana ambaye alianza kupata mafanikio kiasi na ambaye alikua anaonekana ana ndoto kubwa za kuzitimiza.

Kifo ni nini?
Maana ya kawaida ya kifo ni kutengana kwa mwili na roho, wakati mwili unarudi udongoni ulipotwaliwa pia roho hurudi kwa Mungu ilipotoka (Mhubiri 12:7). Kwa Mkristo Mkatoliki maana sahihi zaidi ya kifo ni mwanzo wa maisha ya umilele katika nyumba na meza takatifu ya Bwana. Jambo hili linathibitishwa kaika Mtaguso mkuu wa pili wa Vatikano, hati yake ya liturjia namba 81 na 82 inahitaji uhusiainisho kati ya kifo cha mwanadamu na ufufuko wa Bwana katika ibada za mazishi (Misale ya waumini, Uk 1131).

Kifo kimetoka wapi?
Swali hili ni la msingi sana, mtume Paulo akiwaandikia Warumi (Rum. 5:12-21), anaeleza kuwa dhambi iliingia duniani kupitia Adamu; mtu wa kwanza na kwa kuingia dhambi mauti pia yakaingia, hii ina maana kuwa dhambi ndiyo iliyoleta mauti ulimwenguni, Mungu alimweleza Adamu wazi kuwa siku atakayokaidi amri yake ya kutokula tunda la mti aliomwagizahakika atakufa (Mwanzo 2:17), hii inathibitishwa katika adhabu aliyopewa Adamu (Mwanzo 3:19) kuwa atakula kwa jasho mpaka siku atakaporudi mavumbini alipotwaliwa.

Kila mwanadamu lazima atakufa
Huu ni ukweli ambao wengi hatupendi kuusikia, Ayubu katika mateso yake anakumbuka hili na kusema wazi kuwa kila mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke siku zake duniani ni chache (Ayubu 14:1), kwa kuwa binadamu wote tumerithi dhambi ya asili kutoka kwa Adamu vivyo hivyo tumeirithi adhabu ya kifo, na kwa maana hiyo kila nafsi lazima itaonja mauti. Kwa maana hiyo lazima tukutane na kifo kama tamati ya maisha yetu hapa duniani.

Je tusubiri mauti kwa huzuni?
Hasha! Kwa Mkristu mwenye imani na matumaini kifo si jambo la kutisha, kwani katika kipindi chake chote cha maisha duniani anaishi kwa matumaini kwamba siku moja ataungana na Bwana wetu Yesu Kristo, hivyo hukiangalia kifo kama safari ya kumwendea Yesu katika maisha ya umilele (Katekisimu ya Kanisa Katoiliki: 1020). Huzuni ya kudumu huwa kwa watu wasio na matumaini na imani. Maana siku tunayolala katika mauti duniani, tunaamka katika utukufu kwa Baba yetu mbinguni kwani maisha yetu yote tumeishi tukingoja kwa matumaini kurudi kwake Bwana wetu Yesu Kristu.

 Katika hali ya kawaida ya maisha ya mwanadamu, ndugu, jamaa au rafiki anaposafiri safari ya mbali ambayo itamchukua muda mrefu kurudi huagwa kwa huzuni na matumaini. Familia humuaga huku ikimtakia kila la kheri na huahidi kumwombea arudi salama ili waungane tena pamoja. Huo ndio mfano unaoweza kufananishwa na kifo cha Mkristu. Sisi sote kwa nyakati tofauti lazima tufunge safari ambayo itatutenga na ndugu, jamaa na marafiki zetu, watahuzunika kiasi kwani kwa kitambo kidogo hatutakua nao tena pamoja tukishirikiana katika mambo tuliyozoea kuyafanya pamoja. Lakini saa yaja ambapo sote kwa pamoja tutashiriki meza ya Bwana wetu. Na katika kipindi cha kusubiri wakati huo kufika, tutaendelea kuwasiliana kwa njia ya sala na maombi katika ulimwengu wa roho.

TUJIANDAE KWA KIFO CHEMA

Kifo huja ghafla
Kifo huwa hakipigi hodi, huja mara moja na huja ghafla. Lakini kanisa linatupatia zawadi ya sala za kuomba kifo chema(Tazama sala yenye rehema kamili saa ya kufa, Misale ya waumini Uk. 1089, Sala 15 za Mt. Brigita wa Sweden, Mawaridi ya Sala Uk. 22-26. Pamoja na sala nyenginezo). Sala hizi hutusaidia kujiandaa vyema kukipokea kifo pale kinapokuja. Hutupa matayarisho ya roho zetu kuingia katika uzima wa milele. Zaidi ya yote hutupa matumaini ya kuuona uso wa Bwana.

Baada ya kifo ni hukumu
Baada ya roho na mwili kutengana, mwili hurudi udongoni kwani ndiyo asili yake na roho hurudi kwa Baba ambaye hapo kabla aliipuliza pumzi yake juu ya udongo na kuufanya kiumbe hai. Roho inaporudi kwa Mungu hutoa hesabu juu ya matendo yake duniani na huhukumiwa kutokana na mema na mabaya ambayo ilitenda iliokua duniani (Mathayo 25:31-46).

Hukumu si jambo la kuogopa, ili ni jambo ambalo lazima tulifahamu tunapokua ulimwenguni. Tusisiseme hatutendi maovu kwa kuwa tunaogopa hukumu ya mwisho, ila tusitende maovu kwa kuwa tunao upendo kwa jirani na kwa Mungu. Kutokutenda mabaya kwa sababu unaougopa moto wa milele ni sawa na kusema kama kusingekuwa na moto wa milele ungetenda dhambi. Ni sawa na mwanafunzi ambaye husoma na kufaulu kwa sababu ya kuogopa asiposoma atapata adhabu. Mwanafunzi huyu hatasoma kwa furaha bali kwa machungu. Vivyo hivyo tunapofikiria kuhusu maisha yetu baada ya kifo, tufikirie kuhusu upendo wa Mungu na furaha ya kuungana naye. Tunapowasaidia watu tuwasaidie kwa moyo wa upendo bila kuhesabu kwamba nafanya hivi ili nisiende motoni. Kuyafanya mambo kwa upendo na unyenyekevu ndiyo maana halisi ya moyo uliopondeka ambao Bwana anapenezwa nao (Zaburi 51:17)

Tufanikishe kusudi la Mungu kutuleta Duniani
Kila mwanadamu ambaye Mungu amemleta duniani ana kusudi naye. Kabla ya kuumbwa kwetu na kutungwa mimba alitujua na alikua ameshaweka mipango mema juu yetu (Yeremia 1:5). Hivyo tunapoishi duniani lazima kwanza tulitafute, tulifahamu na tukamilishe kusudi la Mungu kwa sisi kuwapo duniani.

Kila mwanadamu amepewa kusudi la kuutafuta utakatifu na ufalme wa mbingu akiwa hapa duniani. Katika mafundisho yake Bwana wetu Yesu Kristo alitilia mkazo kwamba duniani tunapita na tutilie mkazo kuutafuta ufalme wa mbinguni mengine yatakuja kama ziada (Mathayo 6:33).

Mambo tunayoyafanya duniani yanakusanywa katika hazina yetu mbinguni. Bwana wetu Yesu Kristo anatuasa tuitengeneze hazina mbinguni mahali ambapo roho zetu zitakuapo, tena tusihangaike na hazina za duniani (Mathayo 6:20-21). Hili ni katika kutilia mkazo kuangalia maisha yajayo badala ya kuangalia maisha ya sasa. Mambo ya dunia hutupa raha kwa kipindi kifupi, ni makosa makubwa kuchagua raha ya muda mfupi dhidi ya furaha ya umilele.
Hivyo katika kujiandaa na maisha ya umilele kila jambo tunaloamua kutenda lazima tulitende tukiwa na malengo ya kutimiza lengo la kuufikia utakatifu na ufalme wa Mungu.

Baada ya kutizama lengo hili kuu, kila mwanadamu ana kusudi mahususi ambalo Mungu amemletea duniani. Kusudi hili ni lazima kila mmoja wetu alitafute na alifanikishe. Mfano mzuri ni Bwana wetu Yesu Kristo yeye alitambua ya kuwa kusudi lake kuletwa ulimwenguni ni kuukomboa ulimwengu katika dhambi kwa njia ya kufa msalabani. Aliishi akitambua kusudi hili na ndio maana kabla ya kukata roho alisema, “YAMETIMIA” (Yohana 19:30). Yesu anasema neno hili kubwa akimaanisha yote aliyotumwa, yote yaliyoandikwa na yote yaliyotabiriwa sasa yametimia. Sura ya 17 ya Injili ya Mt. Yohana ni sala ya Kikuhani ambayo Yesu anaitolea mbele ya Mungu Baba, muda mfupi kabla ya mateso na kifo chake, anamueleza kusudi ulilonipa juu ya watu hawa nimelitimiza, sasa Baba umtukuze mwanao. Zawadi anayopokea Bwana wetu Yesu Kristo kwa kazi kubwa hii ni kuketi kuume kwa Baba.

Sisi nasi yatupasa kutimiza makusudi mahususi ambayo Mungu ametuatia. Tunapokiangalia kifo kama njia ya kurudi nyumbani kwa Baba lazima tuatafakari kuhusu kazi Baba aliyotutuma. Tunapozisafisha roho zetu kwa njia ya kitubio pia tukumbuke kutimiza majukumu yetu tuliyopewa na Mungu. Tufanye kila kitu na kila jambo ili wakati wetu wa kuondoka duniani ukifika tuondoke na tabasamu tukisema “YAMETIMIA”. Yatupasa tuondoke tukiwa hatuna deni; tujitafakari na tutafute lipi ni kusudi mahususi la sisi kuwamo duniani na tulitimize.

Tukisubiri kifo kwa matumaini
Baada ya kuchambua yote hayo kwa ufupi na kwa uchache twaweza kubaliana kuwa; kifo ni njia ya mwanadamu kurudi kwa Baba. Pili, roho ya mwan­­­adamu itahukumiwa kutokana na matendo yake ya duniani. Tatu, ili tuwe tayari kwa kifo chema yatupasa kujiandaa kiroho, kimwili na kiakili. Nne, lazima tutimize makusudi ya Mungu kutuleta duniani, kwanza kusudi la jumla la kuufikia uatakatifu kisha kusudi mahususi la kila mmoja wetu. Zaidi ya yote tuwaombee ndugu, jamaa, marafiki na wote wasio na mwombezi ambao wameshatangulia mbele za haki, kama wapo toharani Mungu awapokee katika ufalme wake. Ni vyema tukitizame kifo kwa matumaini ya kumuona tena Mungu.

Maoni

paulo mabula

Mafundisho ni mazuri sana

Frenk Yamola

Amina

Ingia utoe maoni