Jumanne. 26 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumatatu ya 17 ya Mwaka (Jumatatu, Julai 30, 2018)  

Somo la 1

Yer. 13:1–11

Bwana aliniambia hivi, Enenda, ukajinunulie mshipi wa kitani, ukajivike viuno, wala usiutie majini. Basi nikanunua mshipi sawasawa na neno la Bwana, nikajivika viunoni. Nalo neno la Bwana likanijia mara ya pili, kusema, Twaa mshipi ule ulioununua, ulio viunoni mwako, kisha ondoka, enenda mpaka mto Frati, ukauficha karibu na mto Frati, kama Bwana alivyoniamuru. Hata ikawa baada ya siku nyingi, Bwana akaniambia, Ondoka, enenda mpaka mto Frati, ukautwae ule mshipi, niliokuamuru kuuficha huko. Ndipo nikaenda mpaka mto Frati, nikachimba, nikautwaa ule mshipi katika mahali pale nilipouficha; na tazama, mshipi ulikuwa umeharibika, haukufaa, tena kwa lolote. Ndipo neno la Bwana likanijia, kusema, Bwana asema hivi, Jinsi iyo hiyo nitakiharibu kiburi cha Yuda, na kiburi kikuu cha Yerusalemu. Watu hawa waovu, wanaokataa kusikiliza maneno yangu, wanaokwenda kwa ushupavu wa mioyo yao, na kufuata miungu mingine ile kuitumikia na kuiabudu, watakuwa hali moja na mshipi huu, usiofaa kwa lolote. Maana kama vile mshipi unavyoshikamana na viuno vya mtu, ndivyo nilivyowashikamanisha nami nyumba yote ya Israeli, na nyumba yote ya Yuda, asema Bwana; wapate kuwa watu kwangu mimi, na jina, na sifa, na utukufu; lakini hawakutaka kusikia.

Wimbo wa Katikati

Kumb. 32:18–21

Hukumbuki Mwamba aliyekuza,
Mungu aliyekuzaa umemsahau.
Bwana akaona, akawachukia,
Kwa sababu ya kukasirishwa na wanawe na binti zake.
(K) Humkumbuki Mwamba aliyekuzaa.

Akasema, nitawaficha uso wangu,
Nitaona mwisho wao utakuwaje;
Maana, ni kizazi cha ukaidi mwingi,
Watoto wasio imani ndani yao.
(K) Humkumbuki Mwamba aliyekuzaa.

Wamenitia wivu kwa kisicho Mungu,
Wamenikasirisha kwa ubatili wao;
Nami nitawatia wivu kwa wasio watu.
Nami nitawakasirisha kwa taifa lipumbaalo.
(K) Humkumbuki Mwamba aliyekuzaa.

Shangilio

Shangilio

Aleluya, aleluya,
Neno la Kristu likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkimshukuru Mungu Baba kwa Yeye.
Aleluya.

Injili

Mt. 13:31–35

Yesu aliwatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na punje ya haradali, aliyoitwaa mtu akaipanda katika shamba lake; nayo ni ndogo kuliko mbegu zote; lakini ikiisha kumea, huwa kubwa kuliko mboga zote, ikawa mti, hata nyuni wa angani huja na kukaa katika matawi yake. Akawaambia mfano mwingine; Ufalme wa mbinguni umefanana na chachu aliyoitwaa mwanamke, akaisitiri ndani ya pishi tatu za unga, hata ukachachwa wote pia. Hayo yote Yesu aliwaambia makutano kwa mifano; wala pasipo mfano hakuwaambia neno; ili litimie neno lililonenwa na nabii, akisema, Nitafumbua kinywa changu kwa mifano, Nitayatamka yaliyositirika tangu awali.

Maoni


Ingia utoe maoni