Jumanne. 26 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumatano ya 13 ya Mwaka (Jumatano, Julai 04, 2018)  

Somo la 1

Amo. 5:14-15, 21-24

Tafuteni mema, wala si mabaya, mpate kuishi; hivyo Bwana, Mungu wa majeshi, atakuwa pamoja nanyi, kama msemavyo. Yachukieni mabaya; yapendeni mema; mkaithibitishe haki langoni; yamkini kwamba Bwana, Mungu wa majeshi, atawafanyia fadhili mabaki ya Yusufu. Mimi nazichukia sikukuu zenu, asema Bwana nazidharau, nami sitapendezwa na makutano yenu ya dini. Naam, ijapokuwa mnanitolea sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka zenu za unga, sitazikubali; wala sitaziangalia sadaka zenu za amani, na za wanyama walionona. Niondoleeni kelele za nyimbo zenu; kwa maana sitakai kuzisikia sauti za vinanda vyenu. Lakini hukumu na itelemke kama maji, na haki kama maji makuu.

Wimbo wa Katikati

Zab. 50:7 – 13, 16-17

Sikieni, enyi watu wangu, nami nitanena,
Mimi nitakushuhudia, Israeli;
Mimi ndimi niliye Mungu, Mungu wako.
(K) Nitamwonyesha wokovu wa Mungu.

Sitakukemea kwa ajili ya dhabihu zako,
Na kafara zako ziko mbele zangu daima.
Sitatwaa ng’ombe katika nyumba yako,
Wala beberu katika mazizi yako.
(K) Nitamwonyesha wokovu wa Mungu.

Maana kila hayawani ni wangu.
Na makundi juu ya milima elfu.
Nawajua ndege wote wa milima,
Na wanyama wote wa mashamba ni wangu.
(K) Nitamwonyesha wokovu wa Mungu.

Kama ningekuwa na njaa singekuambia,
Maana ulimwengu ni wangu, navyo viujazavyo.
Je! Nile nyama ya mafahali!
Au ninywe damu ya mbuzi.
(K) Nitamwonyesha wokovu wa Mungu.

Maana wewe umechukia maonyo,
Na kuyatupa maneno yangu nyuma yako.
(K) Nitamwonyesha wokovu wa Mungu.

Shangilio

2Kor. 5:19

Aleluya, aleluya,
mungu alikuwa ndani ya Kristu, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, ametia ndani yetu neno la upatanisho.
Aleluya.

Injili

Mt. 8 :28-34

Yesu alipofika ng’ambo katika nchi ya Wagerasi, watu wawili wenye pepo walikutana naye, wanatoka makaburini, wakali mno, hata mtu asiweze kuipitia njia ile. Na tazama, wakapiga kelele, wakisema, Tuna nini nawe, Mwana wa Mungu? Je! Umekuja kututesa kabla ya muhula wetu? Basi, kulikuwako mbali nao kundi la nguruwe wengi wakilisha. Wale pepo wakamsihi, wakisema, Ukitutoa, tuache twende, tukaingie katika lile kundi la nguruwe. Akawaambia, Nendeni. Wakatoka, wakaingia katika nguruwe; na kumbe! Kundi lote wakatelemka kwa kasi gengeni hata baharini, wakafa majini. Lakni wachungaji walikimbia, wakaenda zao mjini, wakazieneza habari zote, na habari za wale wenye pepo pia. Na tazama, mji wote ukatoka kwenda kumlaki Yesu; nao walipomwona, walimsihi aondoke mipakani mwao.

Maoni


Ingia utoe maoni