Masomo ya Misa
Jumamosi ya 12 ya Mwaka (Jumamosi, Juni 30, 2018)
Omb. 2:2, 10 – 14, 18 – 19
Bwana ameyameza makao yote ya Yakobo, wala hakuona huruma; ameziangusha ngome za binti Yuda katika ghadhabu yake; amezibomoa hata nchi ameunajisi ufalme na wakuu wake. Wazee wa binti Sayuni huketi chini, hunyamaza kimya; wametupa mavumbi juu ya vichwa vyao, wamejivika viunoni nguo za magunia; wanawali wa Yerusalemu huinama vichwa vyao kuielekea nchi. Macho yangu yamechoka kwa machozi, mtima wangu umetaabika; ini langu linamiminwa juu ya nchi kwa uharibifu wa binti ya watu wangu; kwa sababu watoto wachanga na wanyonyao, huzimia katika mitaa ya mji. Wao huwauliza mama zao, zi wapi nafaka na divai? Hapo wazimiapo kama waliojeruhiwa katika mitaa ya mji, hapo walipomiminika nafsi zao vifuani mwa mama zao. Nikushuhudie nini? Nikufananishe na nini, ee Binti Yerusalemu? Nikusawazishe na nini, nipate kukufariji, Ee bikira binti Sayuni? Kwa maana uvunjifu wako ni mkuu kama bahari, ni nani awezaye kukuponya? Manabii wako wameona maono kwa ajili yako ya ubatili na upumbavu; wala hawakufunua uovu wako, wapate kurudisha kufungwa kwako; bali wameona mabashiri ya ubatili kwa ajili yako na sababu za kuhamishwa. Mioyo yao ilimlilia Bwana; Ee ukuta wa binti Sayuni! Macho na yachuruzike kama mto mchana na usiku; usijipatie kupumzika; mboni ya macho yako isikome. Inuka, ulalamike usiku, mwanzo wa makesha yake; mimina moyo wako kama maji usoni pa Bwana; umwinulie mikono yako; kwa uhai wa watoto wako wachanga wazimiao kwa njaa, mwanzo wa kila njia kuu.
Zab. 74:1 – 7, 20 – 21 (K) 19
Ee Mungu, mbona umetutupa milele?
Kwa nini hasira yako inatoka moshi
Juu ya kondoo wa malisho yako?
Ulikumbuke kusanyiko lako,
Ulilolinunua zamani.
Ulilolikomboa liwe kabila la urithi wako,
Mlima Sayuni ulioufanya maskani yako.
(K) Usiusahau milele uhai wa watu wako walioonewa.
Upainulie miguu yako palipoharibika milele;
Adui ameufanya kila ubaya katika patakatifu.
Watesi wako wamenguruma kati ya kusanyiko lako;
Wameweka bendera zao ziwe alama.
(K) Usiusahau milele uhai wa watu wako walioonewa.
Wanaonekana kama watu wainuao mashoka,
Waikate miti ya msituni.
Na sasa nakishi yake yote pia
Wanaivunjavunja kwa mashoka na nyundo.
Wamepatia moto patakatifu pako;
Wamelinajisi kao la jina lako hata chini.
(K) Usiusahau milele uhai wa watu wako walioonewa.
Ulitafakari agano;
Maana mahali penye giza katika nchi
Pamejaa makao ya kukatili.
Aliyeonewa asirejee ametiwa haya,
Mnyonge na mhitaji na walisifu jina lako.
(K) Usiusahau milele uhai wa watu wako walioonewa.
Yn. 8:12
Aleluya, aleluya,
Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, asema Bwana, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.
Aleluya.
Mt. 8:5 – 17
Yesu alipoingia Kapernaumu, akida mmoja alimjia, amasihi, akisema, Bwana, mtumishi wangu amelala nyumbani, mgonjwa wa kupooza, anaumwa sana. Yesu akamwambia, Nitakuja, nimponye. Yule akida akamjibu, akasema, Bwana, mimi sistahili wewe uingie chini ya dari yangu, lakini sema neno tu, na mtumishi wangu atapona. Kwa maana mimi nami ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, mwenye askari chini yangu; nikimwambia huyu, Nenda, huenda; na huyu, Njoo, huja; na mtumwa wangu, Fanya hivi, hufanya. Yesu aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia wale waliomfuata, Amin, nawaambieni, Sijaona imani kubwa namna hii, kwa yeyote katika Israeli. Nami nawaambieni, ya kwamba wengi watakuja kutoka mashariki, na magharibi, nao wataketi pamoja na Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo katika ufalme wa mbinguni; bali wana wa ufalme watatupwa katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Naye Yesu akamwambia yule akida, Nenda zako; na iwe kwako kama ulivyoamini. Mtumishi wake akapona saa ile ile. Hata Yesu alipofika nyumbani kwa Petro, akamwona mkwewe Petro, mamaye mkewe, amelala kitandani hawezi homa. Akamgusa mkono, homa ikamwacha; naye akaondoka, akawatumikia. Hata kulipokuwa jioni, wakamletea wengi wenye pepo; akawatoa pepo kwa neno lake, akawaponya wote waliokuwa hawawezi, ili litimie lile neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, na kuyachukua magonjwa yetu.
Maoni
Ingia utoe maoni