Alhamisi. 19 Septemba. 2024

Masomo ya Misa

JUMAPILI YA 4 YA PASAKA, MWAKA C (Jumapili, Aprili 17, 2016)  

Somo la 1

Mdo 13:14, 43-52

Paulo na Barnaba walitoka Perge, wakapita kati ya nchi, wakafika Antiokia, mji wa Pisidia, wakaingia katika sinagogi siku ya sabato, wakaketi. Sinagogi ilipofumukana, Wayahudi na waongofu watauwa wengi wakashikamana na Paulo na Barnaba; ambao, wakisema nao, wakawatia moyo kudumu katika neema ya Mungu. Hata sabato ya pili, watu wengi, karibu mji wote, wakakusanyika walisikie neno la Mungu. Bali Wayahudi walipowaona makutano, wakajaa wivu, wakayakanusha maneno yaliyonenwa na Paulo, wakibisha na kutukana. Paulo na Barnaba wakanena kwa ushujaa wakasema, Ilikuwa lazima neno la Mungu linenwe kwenu kwanza; lakini kwa kuwa mnalisukumia mbali, na kujiona nafsi zenu kuwa hamkustahili uzima wa milele, angalieni, twawageukia Mataifa. Kwa sababu ndivyo tulivyoamriwa na Bwana. Nimekuweka uwe nuru ya Mataifa, Upate kuwa wokovu hata mwisho wa dunia. Mataifa waliposikia hayo wakafurahi, wakalitukuza neno la Bwana, nao waliokuwa wamekusudiwa uzima wa milele wakaamini. Neno la Bwana likaenea katika nchi ile yote. Lakini Wayahudi wakawafitinisha wanawake watauwa wenye cheo na wakuu wa mji, wakawataharakisha watu wawaudhi Paulo na Barnaba; wakawatoa katika mipaka yao, wakaenda Ikonio. Na wanafunzi walijaa furaha na Roho Mtakatifu.

Wimbo wa Katikati

Zab. 100:1-3,5


Mfanyieni Bwana shangwe, dunia yote;
Mtumikieni Bwana kwa furaha;
Njoni mbele zake kwa kuimba.
(K) Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake.

Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu;
Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake;
Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake.
(K) Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake.

Kwa kuwa Bwana ndiye mwema;
Rehema zake ni za milele;
Na uaminifu wake vizazi na vizazi.
(K) Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake.

Somo la 2

Ufu. 7:9, 14b-17

Wakati ule, mimi, Yohane, niliona, na tazama, mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele za Mwana-kondoo, wamevikwa mavazi meupe, wana matawi ya mitende mikononi mwao. Mmoja wa wale wazee akiniambia, Hao ndio wanatoka katika dhiki ile iliyo kuu, nao wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe katika damu ya Mwana-kondoo. Kwa hiyo wako mbele ya kiti cha enzi cha mungu, nao wanamtumikia mchana na usiku katika hekalu lake, na yeye aketiye katika kiti cha enzi atatanda hema yake juu yao. Hawataona njaa tena, wala hawataona kiu tena, wala jua halitawapiga, wala hari iliyo yote. Kwa maana huyo Mwana-kondoo, aliye katikati ya kiti cha enzi, atawachunga, naye atawaongoza kwenye chemchemi za maji yenye uhai, na Mungu atayafuta machozi yote katika macho yao.

Shangilio

Yn. 10:14

Aleluya, aleluya,
Mimi ndimi mchungaji mwema; nao walio wangu nawajua; nao walio wangu wanijua mimi.
Aleluya.

Injili

Yn. 10:27-30

Yesu alisema; Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata. Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu. Baba yangu aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote; wala hakuna mtu awezaye kuwapokonya katika mkono wa Baba yangu. Mimi na Baba tu umoja.

Maoni


Ingia utoe maoni