Masomo ya Misa
Ijumaa ya 5 ya Pasaka (Ijumaa, Mei 04, 2018)
Mdo. 15 : 22-31
Siku zile, baada ya Mtaguso wa Yerusalemu, ikawapendeza mitume na wazee na kanisa lote kuwachagua watu miongoni mwao na kuwapeleka Antiokia pamoja na Paulo na Barnaba; nao ni hawa, Yuda aliyeitwa Barnaba, na Sila, waliokuwa watu wakuu katika ndugu. Wakaandika hivi na kupeleka kwa mikono yao, Mitume na ndugu wazee, kwa ndugu zetu walioko Antiokia na Shamu na Kilikia, walio wa Mataifa; Salamu. Kwa kuwa tumesikia ya kwamba watu waliotoka kwetu wamewasumbua kwa maneno yao, wakipotosha roho zenu, ambao sisi hatukuwaagiza; sisi tumeona vema, hali tumepatana kwa moyo mmoja, kuwachagua watu na kuwapeleka kwenu pamoja na wapendwa wetu Barnaba na Paulo, watu waliohatirisha maisha yao kwa ajili ya jina la Bwana wetu Yesu Kristo. Basi tumewatuma Yuda na Sila, watakaowaambia wenyewe maneno yayo hayo kwa vinywa vyao. Kwa maana ilimpendeza Roho Mtakatifu na sisi, tusiwatwike mzigo ila hayo valiyo lazima, yaani, mjiepushe na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, na nyama zilizosongolewa, na uasherati. Mkijizuia na hayo mtafanya vema. Wasalamu. Hata hao wakiisha kupewa ruhusa wakatelemkia Antiokia; na baada ya kuwakusanyia jamii yote wakawapa ile barua. Nao walipokwisha kuisoma, wakafurahi kwa ajili ya faraja ile.
Zab. 57 : 7-11
Ee Mungu, moyo wangu u thabiti,
Moyo wangu u thabiti.
Nitaimba, nitaimba zaburi,
Amka, utukufu wangu.
Amka, kinanda na kinubi,
Nitaamka alfajiri.
(K) Ee Bwana, nitakushukuru kati ya watu.
au: Aleluya.
Ee Bwana, nitakushukuru kati ya watu,
Nitakuimbia zaburi kati ya mataifa.
Maana fadhili zako ni kubwa hata mbinguni,
Na uaminifu wako hata mawinguni.
Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu,
Na juu ya nchi yote uwe utukufu wako.
(K) Ee Bwana, nitakushukuru kati ya watu.
au: Aleluya.
Yn. 10:27
Aleluya, aleluya,
Kondoo wangu waisikia sauti yangu, nami nawajua, nao wanifuata.
Aleluya.
Yn. 15 :12-17
Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Amri yangu ndiyo hii, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi. Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo. Siwaiti tena watumwa; kwa maana mtumwa hajui atendalo bwana wake; lakini ninyi nimewaita rafiki; kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu. Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni. Haya nawaamuru ninyi, mpate kupendana.
Maoni
Ingia utoe maoni