Masomo ya Misa
Dominika ya 3 ya Pasaka (Jumapili, Aprili 15, 2018)
Mdo. 3:13-15
Petro aliwaambia watu wote: Mungu wa Ibrahimu na wa Isaka na wa Yakobo, Mungu wa baa zetu, amemtukuza mtumishi wake Yesu; ambaye ninyi mlimsaliti na kumkana mbele ya Pilato, alipokuwa ametoa hukumu yake afunguliwe. Bali ninyi mlimkana yule Mtakatifu, yule Mwenye haki, mkataka mpewe mwuaji; mkamwua yule Mkuu wa uzima, ambaye Mungu amemfufua katika wafu; na sisi tu mashahidi wake. Basi sasa, ndugu, najua ya kuwa mliyatenda haya kwa kutokujua kwenu, kama na wakuu wenu walivyotenda. Lakini mambo yale aliyohubiri Mungu tangu zamani kwa kinywa cha manabii wake wote, ya kwamba Kristo wake atateswa, ameyatimiza hivyo. Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe.
Zab. 4:1,3,6,8
Ee Mungu wa haki yangu, uniitikie niitapo;
Umenifanyizia nafasi wakati wa shida;
Unifadhili na kuisikia sala yangu.
(K) Bwana, utuinulie nuru ya uso wako.
Au: Aleluya.
Bali jueni ya kuwa Bwana amejiteulia mtauwa;
Bwana atasikia nimwitapo.
(K) Bwana, utuinulie nuru ya uso wako.
Au: Aleluya.
Wengi husema, Nani atakayetuonyesha mema?
Bwana, utuinulie nuru ya uso wako.
(K) Bwana, utuinulie nuru ya uso wako.
Au: Aleluya.
Katika amani nitajilaza na kupata usingizi mara,
Maaana Wewe, Bwana, peke yako,
Ndiwe unijaliaye kukaa salama.
(K) Bwana, utuinulie nuru ya uso wako.
Au: Aleluya.
1Yoh. 2:1-5a
Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki, naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa dahmbi zetu tu, bali kwa dhambi za ulimwengu wote. Na katika hili twajua ya kuwa tumemjua yeye, ikiwa tunashika amri zake. Yeye asemaye, Nimemjua, wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake. Lakini yeye alishikaye neno lake, katika huyo upendo wa Mungu umekamilika kweli kweli.
Lk. 24:32
Aleluya, aleluya,
Bwana Yesu, utufunulie maandiko; uwashe mioyo yetu unaposema nasi.
Aleluya.
Lk. 24:35-48
Wafuasi waliwapa habari ya mambo yale ya njiani, na jinsi alivyotambulikana nao katika kuumega mkate. Na walipokuwa katika kusema habari hiyo, yeye mwenyewe alisimama katikati yao, akawaambia, Amani iwe kwenu. Wakashituka, wakaogopa sana, wakidhani ya kwamba wanaona roho. Akawaambia, Mbona manafadhaika? Na kwa nini mnaona shaka mioyoni mwenu? Tazameni mikono yangu na miguu yangu, ya kuwa ni mimi mwenyewe. Nishikenishikeni, mwone; kwa kuwa roho haina mwili na mifupa kama mnavyoniona mimi kuwa nayo. Na baada ya kusema hayo aliwaonyesha mikono yake na miguu yake. Basi walipokuwa hawajaamini kwa furaha, huku wakistaajabu, aliwaambia, Mna chakula chochote? Wakampa kipande cha samaki wa kuokwa. Akakitwaa, akala mbele yao. Kisha akawaambia, Hayo ndiyo maneno yangu niliyowaambia nilipokuwa nikali pamoja nanyi, ya kwamba ni lazima yatimizwe yote niliyoandikiwa katika Torati ya Musa, na katika Manabii, na Zaburi. Ndipo akawafunulia akili zao wapate kuelewa na maandiko. Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu, na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu. Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo hayo.
Maoni
Ingia utoe maoni