Masomo ya Misa
Dominika ya 4 ya Kwaresima (Jumapili, Machi 11, 2018)
2 Nya 36:14-16, 19-23
Wakuu wote wa makuhani, na watu, wakakosa mno sawasawa na machukizo yote ya mataifa; wakainajisi nyumba ya Bwana aliyoitakasa katika Yerusalemu. Naye Bwana, Mungu wa baba zao, akatuma kwao kwa mikono ya wajumbe wake, akiondoka mapema, na kutuma; kwa sababu aliwahurumia watu wake, na makao yake; lakini waliwadhihaki wajumbe wa Mungu, na kuyadharau maneno yake, na kuwacheka manabii wake, hata ilipozidi ghadhabu ya Bwana juu ya watu wake, hata kusiwe na kuponya. Wakaiteketeza nyumba ya Mungu, wakaubomoa ukuta wa Yerusalemu, wakayateketeza kwa moto majumba yake yote, wakaviharibu vyombo vyake vyote vya thamani. Na wale waliookoka na upanga akawachukua mpaka Babeli; wakamtumikia yeye na wanawe hata kulipoingia milki ya Uajemi; ili kulitimiza neno la Bwana kwa kinywa cha Yeremia, hata nchi itakapofurahia sabato zake; kwa maana siku zote ilipokaa ukiwa ilishika sabato, kutimiza miaka sabini. Ikawa katika mwaka wa kwanza wa Koreshi, mfalme wa Uajemi, ili kwamba neno la Bwana alilolisema kwa kinywa cha Yeremia lipate kutimizwa, Bwana akamwamsha roho yake Koreshi, mfalme wa Uajemi, hata akapiga mbiu katika ufalme wake wote, akaiandika pia, akisema, Koreshi, mfalme wa Uajemi asema hivi; Bwana, Mungu wa mbinguni, amenipa falme zote za dunia; naye ameniagiza nimjengee nyumba katika Yerusalemu, ulioko Yuda. Basi kila mtu katika ninyi nyote mlio watu wake, Bwana, Mungu wake, na awe pamoja naye, na akwee.
Zab 137:1-6
Kando ya mito ya Babeli ndiko tulikoketi,
Tukalia tulipoikumbuka Sayuni.
Katika miti iliyo katikati yake
Tulivitundika vinubi vyetu.
(K) Ulimi wangu na ugandamane Na kaakaa la kinywa changu, nisipokukumbuka.
Maana huko waliotuchukua mateka
Walitaka tuwaimbie;
Na waliotuonea walitaka furaha;
Tuimbieni baadhi ya nyimbo za Sayuni.
(K) Ulimi wangu na ugandamane Na kaakaa la kinywa changu, nisipokukumbuka.
Tuuimbeje wimbo wa Bwana Katika nchi ya ugeni?
Ee Yerusalemu, nikikusahau wewe,
Mkono wangu wa kuume na usahau.
(K) Ulimi wangu na ugandamane Na kaakaa la kinywa changu, nisipokukumbuka.
Ulimi wangu na ugandamane
Na kaakaa la kinywa changu, nisipokukumbuka.
Nisipoikuza Yerusalemu
Zaidi ya furaha yangu iliyo kuu.
(K) Ulimi wangu na ugandamane Na kaakaa la kinywa changu, nisipokukumbuka.
Efe 2:4-10
Mungu, kwa kuwa ni mwingi wa rehema, kwa mapenzi yake makuu aliyotupenda; hata wakati ule tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa yetu; alituhuisha pamoja na Kristo; yaani, tumeokolewa kwa neema. Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu; ili katika zamani zinazokuja audhihirishe wingi wa neema yake upitao kiasi kwa wema wake kwetu sisi katika Kristo Yesu. Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu. Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo.
Yn 3:16
Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila tu amwaminie awe na uzima wa milele
Yn 3:14-21
Yesu alimwambia Nikedemo: Kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa; ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye. Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu. Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu. Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa. Bali yeye aitendaye kweli huja kwenye nuru, ili matendo yake yaonekane wazi ya kuwa yametendwa katika Mungu.
Maoni
Ingia utoe maoni