Masomo ya Misa
Jumapili ya 2 ya Kwaresima (Jumapili, Februari 25, 2018)
Mwa. 22:1-2, 9a, 10-13, 15-18
Mungu alimjaribu Ibrahimu, akamwambia, Ee Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa. Akasema, Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu yam lima mmojawapo nitakaokuambia. Wakafika mahali pale alipoambiwa na Mungu, Ibrahimu akanyosha mkono wake, akakitwaa kisu ili amchinje mwanawe. Ndipo malaika wa Bwana, akamwita kutoka mbinguni, akasema, Ibrahimu! Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa. Akasema, Usimnyoshee kijana mkono wako, wala usimtendee neno; kwa maana sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee. Ibrahimu akainua macho yake, akaangalia, na tazama, kondoo mume yuko nyuma yake, amenaswa pembe zake katika kichaka. Basi Ibrahimu akaenda akamtwaa huyo kondoo, akamtoa awe sadaka ya kuteketeza badala ya mwanawe. Malaika wa Bwana akamwita Ibrahimu mara ya pili kutoka mbinguni, akasema, Nimeapa kwa nafsi yangu asema Bwana, kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee, katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga uliopo pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao; na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu.
Zab. 116:10, 15-19
Naliamini, kwa maana nitasema,
Mimi naliteswa sana.
Ina thamani machoni pa Bwana,
Mauti ya wacha Mungu wake.
(K) Nitaenenda mbele za Bwana, katika nchi ya walio hai.
Ee Bwana, hakika mimi ni mtumishi wako,
Mtumishi wako, mwana na mjakazi wako,
Umevifungua vifungo vyangu.
Nitakutolea dhabihu ya kushukuru;
Na kulitangaza jina la Bwana.
(K) Nitaenenda mbele za Bwana, katika nchi ya walio hai.
Nitaziondoa nadhiri zangu kwa Bwana,
Naam, mbele ya watu wake wote.
Katika nyua za nyumba ya Bwana,
Ndani yako, Ee Yerusalemu.
(K) Nitaenenda mbele za Bwana, katika nchi ya walio hai.
Rum. 8:31b-34
Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu? Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na Zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye atakayetuombea.
Mt. 17:5
Sauti ya Baba ilitoka katika wingu jeupe: “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, msikieni Yeye.”
Mk. 9:2-9
Yesu akawatwaa Petro na Yakobo, na Yohane, akawaleta juu yam lima mrefu faraghani, peke yao; akageuka sura yake mbele yao; mavazi yake yakimetameta, meupe mno, jinsi asivyoweza dobi duniani kuyafanya meupe. Wakatokewa na Eliya pamoja na Musa, nao walikuwa wakizungumza na Yesu. Petro akajibu, akamwambia Yesu, Rabi, ni vizuri sisi kuwapo hapa; na tufanye vibanda vitatu, kimoja chako wewe, kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya. Maana, hakujua la kunena, kwa kuwa waliingiwa na hofu nyingi. Kisha likatokea wingu, likawatia uvuli; sauti ikatoka katika lile wingu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, msikieni yeye. Mara hiyo walipotazama huku na huku, hawakuona mtu pamoja naoi la Yesu peke yake. Na walipokuwa wakishuka mlimani aliwakataza wasimweleze mtu waliyoyaona, hata Mwana wa Adamu atakapokuwa amefufuka katika wafu.
Maoni
Ingia utoe maoni