Masomo ya Misa
Jumamosi Baada Ya Majivu (Jumamosi, Februari 17, 2018)
Isa. 58:9b-14
Bwana asema hivi: Kama ukiiondoa nira; isiwepo kati yako, wala kunyosha kidole, wala kunena maovu; na kama ukimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi yako, na kuishibisha nafsi iliyoteswa; ndipo nuru yako itakapopambazuka gizani; na kiwi chako kitakuwa kama adhuhuri. Naye Bwana atakuongoza daima, ataishibisha nafsi yako mahali pasipokuwa na maji, na kuitia nguvu mifupa yako; nawe utakuwa kama bustani iliyotiwa maji, na kama chemchemi ambayo maji yake hayapungui. Na watu wako watapajenga mahali palipokuwa ukiwa; utaiinua misingi ya vizazi vingi; nawe utaitwa, Mwenye kutengeneza mahali palipobomoka; na, Mwenye kurejeza njia za kukalia. Kama ukigeuza mguu wako usiihalifu sabato, usifanye anasa yako siku ya utakatifu wangu; ukiita sabato siku ya furaha, na siku takatifu ya Bwana yenye heshima; ukiitukuza, kwa kutokuzifanya njia zako mwenyewe, wala kuyatafuta yakupendezayo wala kusema maneno yako mwenyewe; ndipo utakapojifurahisha katika Bwana; nami nitakupandisha mahali pa nchi palipoinuka; nitakulisha urithi wa Yakobo baba yako; kwa maana kinywa cha Bwana kimenena hayo.
Zab. 86:1-2, 3-4, 5-6
Ee Bwana, utege sikio lako unijibu,
Maana mimi ni maskini na mhitaji,
Unihifadhi nafsi yangu,
Maana mimi ni mcha Mungu.
Wewe uliye Mungu wangu,
Umwokoe mtumishi wako anayekutumaini.
(K) Ee Bwana, unifundishe njia yako; Nitakwenda katika kweli yako.
Wewe, Bwana, unifadhili,
Maana nakulilia Wewe mchana kutwa.
Uifurahishe nafsi ya mtumishi wako,
Maana nafsi yangu nakuinulia Wewe, Bwana.
(K) Ee Bwana, unifundishe njia yako; Nitakwenda katika kweli yako.
Kwa maana Wewe, Bwana, U mwema,
Umekuwa tayari kusamehe,
Na mwingi wa fadhili,
Kw awatu wote wakuitao.
Ee Bwana, uyasikie maombi yangu;
Uisikilize sauti ya dua zangu.
(K) Ee Bwana, unifundishe njia yako; Nitakwenda katika kweli yako.
Eze. 33:11
Waambie, kama mimi niishivyo, asema Bwana Mungu, Sikufurahii kufa kwake mtu mwovu; Bali aghairi mtu mwovu, na kuiacha njia yake akaishi.
Lk. 5:27-32
Siku ile: Yesu akaona mtoza ushuru, jina lake Lawi, ameketi forodhani, akamwambia, Nifuate. Akaacha vyote, akaondoka, akamfuata. Na Lawi akamfanyia karamu kubwa nyumbani mwake; palikuwa na mkutano mkuu wa watoza ushuru na watu wengineo waliokuwa wameketi chakulani pamoja nao. Ikawa Mafarisayo na waandishi wao kuwanung’unukia wanafunzi wake, wakisema, Mbona mnakula na kunywa pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi? Yesu akajibu akawaambia, Wenye afya hawana haja na tabibu, isipokuwa walio hawawezi. Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi, wapate kutubu.
Maoni
Ingia utoe maoni