Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Alhamisi Baada Ya Majivu (Alhamisi, Februari 15, 2018)  

Somo la 1

Kum. 30:15-20

Musa aliwaambia watu akisema: Aangalia, nimekuwekea leo mbele yako uzima na mema, na mauti na mabaya; kwa hivi nikuagizavyo leo kumpenda Bwana, Mungu wako, kuenenda katika njia zake, na kushika maagizo yake, na amri zake, na hukumu zake, upate kuwa hai na kuongezeka; Bwana, Mungu wako, apate kukubarikia katika nchi uingiayo kuimiliki. Lakini moyo wako ukikengeuka, usipotaka kusikiza, lakini ukavutwa kando kwenda kuabudu miungu mingine, na kuitumikia; nawahubiri hivi leo hakika mtaangamia; hamtazifanya siku zenu kuwa nyingi juu ya nchi, uivukiayo Yoradani, uingie kuimiliki. Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti Baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako; kupenda Bwana, Mungu wako, kuitii sauti yake, na kushikamana naye; kwani hiyo ndiyo uzima wako, na wingi wa siku zako; upate kukaa katika nchi Bwana aliyowaapia baba zako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kuwa atawapa.

Wimbo wa Katikati

Zab. 1:1-4, 6

Heri mtu yule asiyekwenda
Katika shauri la wasio haki;
Wala hakusimama katika njia ya wakosaji;
Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.
Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo,
Na sheria yake huitafakari mchana na usiku.
(K) Heri mtu aliyemfanya Bwana kuwa tumaini lake.

Naye atakuwa kama mti ulipopandwa
Kandokando ya vijito vya maji,
Uzaao matunda yake kwa majira yake,
Wala jani lake halinyauki;
Na kila alitendalo litafanikiwa.
(K) Heri mtu aliyemfanya Bwana kuwa tumaini lake.

Sivyo walivyo wasio haki;
Hao ni kama makapi yapeperushayo na upepo.
Kwa kuwa Bwana anaijua njia ya wenye haki,
Bali njia ya wasio haki itapotea.
(K) Heri mtu aliyemfanya Bwana kuwa tumaini lake.

Shangilio

Zab. 130:5

Nimemgnoja Bwana, roho yangu imengoja, na neno lake nimelitumaini. Nafsi yangu inamngoja Bwana, kuliko walinzi waingojavyo asubuhi, naam, walinzi waingojao asubuhi.

Injili

Lk. 9:22-25

Siku ile: Yesu aliwaambia wafuasi wake kwamba imempasa Mwana wa Adamu kupata mateso mengi na kukataliwa na wazee na wakuu wa makuhani na waandishi, na kuuawa na siku ya tatu kufufuka. Akawaambia wote, Mtu yeyote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha. Kwa kuwa yamfaa nini mtu kuupata ulimwengu wote, kama akijiangamiza, na kujipoteza mwenyewe?

Maoni


Ingia utoe maoni