Masomo ya Misa
Dominika ya 6 ya Mwaka (Jumapili, Februari 11, 2018)
Law. 13;1-2, 44-46
Bwana alinena na Musa na Haruni, na kuwaambia, Mtu atakapokuwa na kivimbe katika ngozi ya mwili wake, au kikoko, au kipaku king’aacho, nalo likawa pigo la ukomma katika ngozi ya mwili wake, ndipo atakapoletwa kwa Haruni kuhani, au kwa wanawe, makuhani mmojawapo; yeye ni mtu mwenye ukoma, yu najisi; na kuhani hana budi atasema kuwa yu najisi; pigo lake li katika kichwa chake. Kisha mwenye ukoma aliye na pigo ndani yake, nguo zake zitararuliwa, na nywele za kichwa chake zitaachwa wazi, naye atafunika mdomo wake wa juu, naye atapiga kelele, Ni najisi, ni najisi. Siku zote ambazo pigo li ndani yake, yeye atakuwa mwenye unajisi; yeye yu najisi; atakaa peke yake; makazi yake yatakuwa nje ya marago.
Zab. 32:1-2, 5, 11 (K) 7
Heri aliyesamehewa dhambi,
Na kusitiriwa makosa yake.
Heri Bwana asiyemhesabia upotovu,
Ambaye rohoni mwake hamna hila.
(K) Ndiwe sitara yangu, utanihifadhi na mateso, utanizungusha nyimbo za wokovu.
Nalikujulisha dhambi yangu,
Wala sikuuficha upotovu wangu.
Nalisema, Nitayakiri maasi yangu kwa Bwana,
Nawe ukanisamehe upotovu wa dhambi yangu.
(K) Ndiwe sitara yangu, utanihifadhi na mateso, utanizungusha nyimbo za wokovu.
Mfurahieni Bwana;
Shangilieni, enyi wenye haki.
Pigeni vigelegele vya furaha;
Ninyi nyote mlio wanyofu wa moyo.
(K) Ndiwe sitara yangu, utanihifadhi na mateso, utanizungusha nyimbo za wokovu.
1Kor. 10:31-33, 11:1
Ndugu, mlapo, au mnywapo, au mtendapo neno lolote, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu. Msiwakoseshe Wayahudi wala Wayunani wala kanisa la Mungu; vile vile kama mimi niwapendezavyo watu wote katika mambo yote, nisitake faida yangu mwenyewe, ila faida yao walio wengi, wapate kuokolewa. Mnifuate mimi kama mimi ninavyomfuata Kristo.
Lk. 19:38
Aleluya, aleluya,
Ndiye mbarikiwa Mfalme ajaye kwa jina la Bwana; Amani mbinguni, na utukufu huko juu.
Aleluya.
Mk. 1:40-45
Akaja kwake mtu mwenye ukoma, akamsihi na kumpigia magoti, na kumwambia, Ukitaka, waweza kunitakasa. Naye akamhurumia, akanyosha mkono wake, akamgusa, akamwambia, Nataka, takasika. Na mara ukoma wake ukamtoka, akatakasika. Akamwambia, Angalia, usimwambie mtu neno lolote, ila enenda zako ukajionyeshe kwa kuhani, ukatoe alivyoamuru Musa kwa kutakasika kwako, iwe ushuhuda kwao. Lakini akatoka, akaanza kuhubiri maneno mengi, na kulitangaza lile neno, hata Yesu asiweze tena kuingia mjini kwa wazi; bali alikuwako nje mahali pasipokuwa na watu, wakamwendea kutoka kila mahali.
Maoni
Ingia utoe maoni