Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumatatu ya 3 ya Mwaka (Jumatatu, Januari 22, 2018)  

Somo la 1

2 Sam 5:1-7, 10

Kabila zote za Israeli wakamwendea Daudi huko Hebroni, wakasema naye, wakinena, Tazama, sisi tu mfupa wako na nyama yako. Zamani za kale, hapo Sauli alipokuwa mfalme juu yetu, wewe ndiwe uliyewaongoza Israeli watoke nje, na kuingia ndani. Naye Bwana akakuambia, Wewe utawalisha watu wangu Israeli, nawe utakuwa mkuu juu ya Israeli. Basi wazee wote wa Israeli wakamwendea mfalme huko Hebroni, naye mfalme Daudi akapatana nao huko Hebroni mbele za Bwana; wakamtia Daudi mafuta awe mfalme juu ya Israeli. Daudi alikuwa amepata miaka thelathini alipoanza kutawala, akatawala miaka arobaini. Huko Hebroni alitawala miaka saba na miezi sita; na katika Yerusalemu alitawala miaka thelathini na tatu juu ya Israeli wote na Yuda. Kisha mfalme na watu wake wakaenda Yerusalemu ili kupigana na Wayebusi, wenyeji wa nchi ile; hao ndio waliomwambia Daudi, wakisema, Usipowaondoa vipofu, na viwete, hutaingia humu kamwe; huku wakidhania ya kuwa Daudi hawezi kuingia humo. Lakini Daudi aliipiga ngome ya Sayuni; huu ndio mji wa Daudi. Naye Daudi akazidi kuwa mkuu; kwa maana Bwana, Mungu wa majeshi, alikuwa pamoja naye.

Wimbo wa Katikati

Zab 89:19-21, 24-25

Ndipo ulipowaambia watakatifu wako kwa njozi, 

Ukasema, nimempa aliye hodari msaada; 

Nimemtukuza aliyechaguliwa miongoni mwa watu. 

(K) Uaminifu wangu na fadhili zangu atakuwa nazo.


Nimemwona Daudi, mtumishi wangu, 

Nimempaka mafuta yangu matakatifu. 

Ambaye mkono wangu utakuwa thabiti kwake, 

Na mkono wangu utamtia nguvu.

(K) Uaminifu wangu na fadhili zangu atakuwa nazo.


Uaminifu wangu na fadhili zangu atakuwa nazo, 

Na kwa jina langu pembe yake itatukuka. 

Nitaweka mkono wake juu ya bahari, 

Na mkono wake wa kuume juu ya mito. 

(K) Uaminifu wangu na fadhili zangu atakuwa nazo.

Injili

Mk 3:22-30

Waandishi walioshuka kutoka Yerusalemu wakasema, Ana Beelzebuli, na, Kwa mkuu wa pepo huwatoa pepo. Akawaita, akawaambia kwa mifano, Awezaje Shetani kumtoa Shetani? Na ufalme ukifitinika juu ya nafsi yake, ufalme huo hauwezi kusimama; na nyumba ikifitinika juu ya nafsi yake, nyumba hiyo haiwezi kusimama. Na kama Shetani ameondoka juu ya nafsi yake, akafitinika, hawezi kusimama, bali huwa na kikomo. Hawezi mtu kuingia ndani ya nyumba ya mtu mwenye nguvu, na kuviteka vitu vyake, asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu; ndipo atakapoiteka nyumba yake. Amin, nawaambia, Dhambi zote watasamehewa wanadamu, na kufuru zao watakazokufuru zote; bali mtu atakayemkufuru Roho Mtakatifu hana msamaha hata milele; ila atakuwa ana dhambi ya milele, kwa vile walivyosema, Ana pepo mchafu.

Maoni


Ingia utoe maoni