Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 3 ya Mwaka (Jumapili, Januari 21, 2018)  

Somo la 1

Yon 3:1-5,10

Neno la Bwana likamjia Yona mara ya pili, kusema, Ondoka, uende Ninawi, mji ule mkubwa; ukaihubiri habari nitakayokuamuru. Basi Yona akaondoka, akaenda Ninawi, kama Bwana alivyonena. Basi Ninawi ulikuwa mji mkubwa mno, ukubwa wake mwendo wa siku tatu. Yona akaanza kuuingia mji mwendo wa siku moja, akapaza sauti yake, akasema, Baada ya siku arobaini Ninawi utaangamizwa. Basi watu wa Ninawi wakamsadiki Mungu; wakatangaza kufunga, wakajivika nguo za magunia, tangu yeye aliye mkubwa hata aliye mdogo. Mungu akaona matendo yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya. Basi Mungu akalighairi neno lile baya, ambalo alisema atawatenda; asilitende.


Wimbo wa Katikati

Zab 25:4-9

Ee Bwana, unijulishe njia zako, 

Unifundishe mapito yako, 

Uniongoze katika kweli yako, Na kunifundisha. 

Maana Wewe ndiwe Mungu wa wokovu wangu. 

(K) Ee Bwana unijulishe njia zako.


Ee Bwana, kumbuka rehema zako na fadhili zako, 

Maana zimekuwako tokea zamani. 

Usiyakumbuke makosa ya ujana wangu, Wala maasi yangu. 

Unikumbuke kwa kadiri ya fadhili zako, 

Ee Bwana kwa ajili ya wema wako. 

(K) Ee Bwana unijulishe njia zako.


Bwana yu mwema, mwenye adili, 

Kwa hiyo atawafundisha wenye dhambi njia. 

Wenye upole atawaongoza katika hukumu, 

Wenye upole atawafundisha njia yake.

(K) Ee Bwana unijulishe njia zako.

Somo la 2

1 Kor 7:29-31

Lakini, ndugu, nasema hivi, muda ubakio si mwingi; basi tokea sasa wale walio na wake na wawe kama hawana; na wale waliao kama hawalii; na wale wafurahio kama hawafurahi; na wale wanunuao, kama hawana kitu. Na wale wautumiao ulimwengu huu, kama hawautumii sana; kwa maana mambo ya ulimwengu huu yanapita.

Shangilio

Mk 1:15

Aleluya, aleluya,

Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni na kuiamini Injili.

Aleluya

Injili

Mk 1:11-20

Hata baada ya Yohana kutiwa gerezani, Yesu akaenda Galilaya, akiihubiri Habari Njema ya Mungu, akisema, Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili. Naye alipokuwa akipita kando ya bahari ya Galilaya, akamwona Simoni na Andrea nduguye, wakitupa jarife baharini; kwa maana walikuwa wavuvi. Yesu akawaambia, Njoni mnifuate, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu. Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata. Akaendelea mbele kidogo, akamwona Yakobo wa Zebedayo, na Yohana nduguye, nao pia walikuwa chomboni, wakizitengeneza nyavu zao. Mara akawaita, wakamwacha baba yao Zebedayo ndani ya chombo pamoja na watu wa mshahara, wakaenda, wakamfuata. 


Maoni


Ingia utoe maoni