Masomo ya Misa
Ijumaa ya 2 ya Mwaka (Ijumaa, Januari 19, 2018)
1 Sam 24:2-20
Sauli alitwaa watu elfu waliochaguliwa katika Israeli wote, akaenda kumtafuta Daudi na watu wake juu ya majabali ya mbuzi-mwitu. Akafika penye mazizi ya kondoo kando ya njia, na huko kulikuwa na pango; Sauli akaingia ndani ili kuifunika miguu. Na Daudi na watu wake walikuwa wakikaa mle pangoni ndani sana. Nao watu wa Daudi wakamwambia, Tazama, hii ndiyo siku ile aliyokuambia Bwana, Angalia, nitamtia adui yako mikononi mwako, nawe utamtenda yo yote utakayoona kuwa mema. Basi Daudi akainuka, akaukata upindo wa vazi lake Sauli kwa siri. Lakini halafu, moyo wake Daudi ukamchoma, kwa sababu amekata upindo wa vazi lake Sauli. Akawaambia watu wake, Hasha! Nisimtendee bwana wangu, masihi wa BWANA,neon hili,kuunyosha mkono wangu juu yake,kwa maana yeye ni masihi wa BWANA. Basi Daudi akawazuia watu wake kwa maneno hayo, asiwaache kumwondokea Sauli. Kisha Sauli akatoka pangoni, akaenda zake. Daudi naye akainuka baadaye, akatoka pangoni, akamwita Sauli, akisema, Bwana wangu, mfalme. Na Sauli alipotazama nyuma, Daudi akainama uso wake hata nchi, akamsujudia. Daudi akamwambia Sauli, Kwa nini unasikiliza maneno ya watu wasemao, Tazama, Daudi anataka kukudhuru? Tazama, leo hivi macho yako yameona jinsi Bwana alivyokutia mikononi mwangu pangoni, na watu wengine wakaniambia nikuue; lakini nikakuacha; nikasema, Sitaki kuunyosha mkono wangu juu ya bwana wangu; kwa maana yeye ni masihi wa BWANA. Tena, baba yangu, tazama, tafadhali, tazama upindo wa vazi lako mkononi mwangu; maana ikiwa nimeukata upindo wa vazi lako, nisikuue, ujue, na kuona ya kuwa hakuna uovu wala kosa mkononi mwangu, wala sikukukosa neno; ingawa wewe unaniwinda roho yangu ili kuikamata. Bwana atuamue, mimi na wewe, na Bwana anilipizie kisasi changu kwako; lakini mkono wangu hautakuwa juu yako. Kama vile walivyosema watu wa kale katika mithali yao, Katika waovu hutoka uovu; ila mkono wangu hautakuwa juu yako. Na mfalme wa Israeli ametoka ili kumfuatia nani? Unamwinda nani? Ni kuwinda mbwa mfu, au kiroboto. Basi Bwana atuamue, akatuhukumu mimi na wewe, akaone, akanitetee neno langu, akaniokoe na mkono wako. Ikawa, Daudi alipokwisha kumwambia Sauli maneno hayo Sauli alisema, Hii ndiyo sauti yako, Daudi, mwanangu? Naye Sauli akapaza sauti yake, akalia. Akamwambia Daudi, Wewe u mwenye haki kuliko mimi; maana wewe umenitendea mema, nami nimekutenda mabaya. Nawe umeonyesha leo jinsi ulivyonitendea mema, kwani Bwana aliponitia mikononi mwako, hukuniua. Maana mtu akimwona adui yake, je! Atamwacha aende zake salama? Basi Bwana na akulipe mema kwa haya uliyonitendea leo. Na sasa, angalia, najua ya kuwa hakika utakuwa mfalme, na ufalme wa Israeli utafanyika imara mkononi mwako.
Zab 57:1-3, 5, 11
Unirehemu, Ee Mungu, unirehemu mimi,
Maana nafsi yangu imekukimbilia Wewe.
Nitaukimbilia uvuli wa mbawa zako,
Hata misiba hii itakapopita.
(K) Unirehemu, Ee Mungu, unirehemu mimi.
Nitamwita MUNGU Aliye juu,
Mungu anitimiziaye mambo yangu.
Atapeleka toka mbinguni na kuniokoa,
Atukanapo yule atakaye kunimeza.
Mungu atazipeleka Fadhili zake na kweli yake
(K) Unirehemu, Ee Mungu, unirehemu mimi.
Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu,
Na juu ya nchi yote uwe utukufu wako.
Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu,
Na juu ya nchi yote uwe utukufu wako.
(K) Unirehemu, Ee Mungu, unirehemu mimi.
Mk 3:13-19
Yesu alipanda mlimani, akawaita aliowataka mwenyewe; wakamwendea. Akaweka watu kumi na wawili, wapate kuwa pamoja naye, na kwamba awatume kuhubiri, tena wawe na amri ya kutoa pepo. Akawaweka wale Thenashara; na Simoni akampa jina la Petro; na Yakobo, mwana wa Zebedayo, na Yohana nduguye Yakobo, akawapa jina la Boanerge, maana yake, wana wa ngurumo; na Andrea, na Filipo, na Bartholomayo, na Mathayo, na Tomaso, na Yakobo wa Alfayo, na Thadayo, na Simoni Mkananayo, na Yuda Iskariote, ndiye aliyemsaliti.
Maoni
Ingia utoe maoni