Masomo ya Misa
Jumatatu ya 2 ya Mwaka (Jumatatu, Januari 15, 2018)
1Sam. 15:16-23
Samweli alimwambia Sauli, Ngoja, nami nitakuambia neno aliloniambia Bwana usiku huu. Naye akamwambia, Haya, sema. Basi Samweli akasema, Ingawa ulikuwa mdogo machoni pako mwenyewe, je! Hukufanywa kuwa kichwa cha kabila za Israeli? Naye Bwana akakutia mafuta uwe mfalme wa Israeli. Kisha Bwana akakutuma safarini, akasema, Enenda ukawaangamize kabisa wale Waamaleki wenye dhambi, upigane nao hata watakapoangamia. Mbona, basi, hukuitii sauti ya Bwana, bali ukazirukia nyara ukafanya yaliyo maovu machoni pa Bwana.
Sauli akamwambia Samweli, Hakika mimi nimeitii sauti ya Bwana, nami nimemleta Agagi, mfalme wa Waamaleki, tena nimewaangamiza Waamaleki kabisa. Ila watu waliteka nyara, kondoo na ng’ombe walio wazuri, katika vitu vilivyowekwa wakfu, kusudi wavitoe dhabihu kwa Bwana, Mungu wako, huko Gilgali.
Naye Samweli akasema, Je! Bwana huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu, sawasawa na dhabihu, na kusikia kuliko mafuta ya beberu. Kwani kuasi ni kama dhambi ya uchawi, na ukaidi ni kama ukafiri na vinyago; kwa kuwa umelikataa neno la Bwana, Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme.
Zab. 50:8-9, 16-17, 21, 23
Sitakukemea kwa ajili ya dhabihu zako,
Na kafara zako ziko mbele zangu daima.
Sitatwaa ng’ombe katika nyumba yako,
Wala bebeeru katika mazizi yako.
(K) Nitamwonyesha wokovu wa Mungu.
Una nini wewe kuitangaza sheria yangu,
Na kuliweka agano langu kinywani mwako?
Maana wewe umechukia maonyo,
Na kuyatupa maneno yangu nyuma yako.
(K) Nitamwonyesha wokovu wa Mungu.
Ndivyo ulivyofanya, nami nitanyamaza;
Ukadhani ya kuwa Mimi ni kama wewe.
Atoaye dhabihu za kushukuru,
Ndiye atakayenitukuza.
Naye autengenezaye mwenendo wake,
Nitamwonyesha wokovu wa Mungu.
(K) Nitamwonyesha wokovu wa Mungu.
Zab. 147:12,15
Aleluya, aleluya,
Msifu Bwana, Ee Yerusalemu, huipeleka amri yake juu ya nchi.
Aleluya.
Mk. 2:18-22
Siku moja wanafunzi wake Yohane na Mafarisayo walikuwa wakifunga; basi walikuja, wakamwambia, Kwani wanafunzi wa Yohane na wanafunzi wa Mafarisayo hufunga, bali wanafunzi wako hawafungi?
Yesu akawaambia, Walioalikwa arusini wawezaje kufunga maadamu bana-arusi yupo pamoja nao? Muda wote walipo na bwana-arusi pamoja nao hawawezi kufunga. Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana-arusi, ndipo watakapofunga siku ile. Hakuna mtu ashonaye kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu; ikiwa ashona, kile kipya kilichotiwa huliharibu lile vazi kuukuu, na pale palipotatuka huzidi. Wala hakuna mtu atiaye divai mpya katika viriba vikuukuu; ikiwa atia, ile divai mpya itavipasua viriba vile, divai ikamwagika, vile viriba vikaharibika. Bali hutia divai mpya katika viriba vipya.
Maoni
Ingia utoe maoni