Masomo ya Misa
Dominika ya 2 ya Mwaka (Jumapili, Januari 14, 2018)
1 Sam 3:3b-10, 19
Samweli alikuwa amelala katika hekalu la Bwana, palipokuwa na sanduku la Mungu; basi, wakati huo Bwana akamwita Samweli; naye akasema, Mimi hapa. Akamwendea Eli kwa haraka, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Akasema, Sikukuita; kalale tena. Naye akaenda, akalala tena. Bwana akaita mara ya pili, Samweli! Samweli! Akaondoka akamwendea Eli, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Akajibu, Sikukuita, mwanangu; kalale tena. Basi Samweli alikuwa hamjui Bwana bado, na neno la Bwana lilikuwa bado halijafunuliwa kwake. Bwana akamwita Samweli mara ya tatu. Naye akaondoka akamwendea Eli, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Ndipo Eli akatambua ya kuwa Bwana ndiye aliyemwita yule mtoto. Kwa hivyo Eli akamwambia Samweli, Enenda, kalale; itakuwa, akikuita, utasema, Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi wako anasikia. Basi Samweli akaenda akalala mahali pake. Bwana akaja, akasimama, akaita vile vile kama kwanza, Samweli! Samweli! Ndipo Samweli akasema, Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi wako anasikia. Samweli akakua, naye Bwana alikuwa pamoja naye, wala hakuliacha neno lake lo lote lianguke chini.
Zab 40:1,3,6-9
Nalimngoja Bwana kwa saburi,
Akaniinamia akakisikia kilio changu.
Akatia wimbo mpya kinywani mwangu,
Ndio sifa zake Mungu wetu.
(K) Ndipo niliposema, tazama nimekuja, kufanya mapenzi yako.
Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo,
Masikio yangu umeyazibua,
Kafara na sadaka za dhambi hukuzitaka.
Ndipo niliposema, Tazama nimekuja,
(K) Ndipo niliposema, tazama nimekuja, kufanya mapenzi yako.
Katika gombo la chuo nimeandikiwa,
Kuyafanya mapenzi yako, Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu;
Naam, sheria yako imo moyoni mwangu.
(K) Ndipo niliposema, tazama nimekuja, kufanya mapenzi yako.
Nimehubiri habari za haki katika kusanyiko kubwa.
Sikuizuia midomo yangu; Ee Bwana, unajua.
(K) Ndipo niliposema, tazama nimekuja, kufanya mapenzi yako.
1 Kor 6:13c-15a, 17-20
Mwili si kwa zinaa, bali ni kwa Bwana, naye Bwana ni kwa mwili. Naye Mungu alimfufua Bwana, na tena atatufufua sisi kwa uweza wake. Je! Hamjui ya kuwa miili yenu ni viungo vya Kristo? Basi nivitwae viungo vya Kristo na kuvifanya viungo vya kahaba? Lakini yeye aliyeungwa na Bwana ni roho moja naye. Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe. Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe; maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu.
Mt 11:25
Aleluya,aleluya
Wakati ule Yesu akajibu akasema;
Nakushukuru Baba Bwana wa mbingu na nchi kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili ukawafunulia watoto wachanga.
Aleluya.
Yn 1:35-42
Yohana alikuwa amesimama pamoja na wawili katika wanafunzi wake. Akamtazama Yesu akitembea, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu! Wale wanafunzi wawili wakamsikia akinena, wakamfuata Yesu. Yesu aligeuka, akawaona wakimfuata, akawaambia, Mnatafuta nini? Wakamwambia, Rabi, (maana yake, Mwalimu), unakaa wapi? Akawaambia, Njoni, nanyi mtaona. Wakaenda, wakaona akaapo, wakakaa kwake siku ile. Nayo ilikuwa yapata saa kumi. Andrea, nduguye Simoni Petro, alikuwa mmoja wa wale wawili waliomsikia Yohana na kumfuata Yesu. Huyo akamwona kwanza Simoni, ndugu yake mwenyewe, akamwambia, Tumemwona Masihi (maana yake, Kristo). Akampeleka kwa Yesu. Naye Yesu akamtazama, akasema, Wewe u Simoni, mwana wa Yohana; nawe utaitwa Kefa (tafsiri yake Petro, au Jiwe).
Maoni
Ingia utoe maoni