Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 4 ya Majilio (Jumapili, Desemba 24, 2017)  

Somo la 1

2 Sam 7: 1-5, 8-11, 16

Ikawa, mfalme alipokuwa akikaa katika nyumba yake, hapo BWANA alipomstarehesha, asiudhiwe na adui zake waliomzunguka pande zote, mfalme akamwambia Nathani, nabii, Angalia sasa, mimi ninakaa katika nyumba ya mierezi, bali sanduku la Mungu linakaa ndani ya mapazia. Nathani akamwambia mfalme, Haya, fanya yote yaliyomo moyoni mwako; maana BWANA yu pamoja nawe. Ikawa usiku uo huo, neno la BWANA likamfikia Nathani kusema, Enenda, ukamwambie mtumishi wangu, Daudi, BWANA asema hivi, Je! Wewe utanijengea nyumba, nikae ndani yake? Basi, sasa, mwambie mtumishi wangu, Daudi, maneno haya, BWANA wa majeshi asema hivi, Nalikutwaa katika zizi la kondoo, katika kuwaandama kondoo, ili uwe mkuu juu ya watu wangu, juu ya Israeli; nami nimekuwa pamoja nawe kila ulikokwenda, na kuwakatilia mbali adui zako wote mbele yako; nami nitakufanyia jina kuu, kama jina la wakuu walioko duniani. Tena nitawaagizia mahali watu wangu Israeli, nami nitawapanda, wapate kukaa mahali pao wenyewe, wasiondolewe tena; wala wana wa uovu hawatawatesa tena, kama hapo kwanza; naam, kama vilivyokuwa tangu siku ile nilipowaamuru waamuzi, wawe juu ya watu wangu Israeli; nami nitakustarehesha mbele ya adui zako wote.Tena BWANA anakuambia ya kwamba BWANA atakujengea nyumba.

Na nyumba yako, na ufalme wako, vitathibitishwa milele mbele yako. Nacho kiti chako kitafanywa imara milele. 


Wimbo wa Katikati

Zab 89: 1-4, 26, 28

Fadhili za BWANA nitaziimba milele;

Kwa kinywa changu nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wako.

Maana nimesema, 

Fadhili zitajengwa milele;

Katika mbingu utauthibitisha uaminifu wako.

(K) Fadhili za BWANA nitaziimba milele


Nimefanya agano na mteule wangu,

Nimemuapia Daudi, mtumishi wangu.

Wazao wako nitawafanya imara milele,

Nitakijenga kiti chako cha enzi hata milele.

(K) Fadhili za BWANA nitaziimba milele 


Yeye ataniita, Wewe baba yangu,

Mungu wangu na mwamba wa wokovu wangu.

Hata milele nitamwekea fadhili zangu,

Na agano langu litafanyika amini kwake.

(K) Fadhili za BWANA nitaziimba milele

Somo la 2

Rum 16: 25 - 27

Sasa na atukuzwe yeye awezaye kuwafanya imara, sawasawa na injili yangu na kwa kuhubiriwa kwake Yesu Kristo, sawasawa na ufunuo wa ile siri iliyositirika tangu zamani za milele, ikadhihirishwa wakati huu kwa maandiko ya manabii, ikajulikana na mataifa yote kama alivyoamuru Mungu wa milele, ili waitii Imani.Ndiye Mungu mwenye hekima peke yake. Utukufu una yeye kwa Yesu Kristo, milele na milele, Amina. 


Shangilio

Lk 1: 38

Aleluya aleluya

Mariamu akasema,  Tazama mimi ni mjakazi wa Bwana; Na iwe kwangu kama ulivyosema.

Kisha malaika akaondoka akaenda zake 

Aleluya

Injili

Lk 1:26 - 38

Malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti, kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake bikira huyo ni Mariamu. Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe. Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani? Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho. Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu. Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu. Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka akaenda zake.


Maoni


Ingia utoe maoni