Masomo ya Misa
Jumatano ya 1 ya Majilio (Jumatano, Desemba 06, 2017)
Isa. 25:6-10
Siku ile Bwana wa majeshi atawafanyia mataifa yote karamu ya vitu vinono, karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wake, karamu ya vinono vilivyojaa mafuta, karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wake, iliyochujwa sana. Naye katika mlima huu atauharibu uso wa sitara iliyowekwa juu ya watu wote, na utaji ule uliotandwa juu ya mataifa yote. Amemeza mauti hata milele; na Bwana Mungu atafuta machozi katika nyuso zote; na aibu ya watu wake ataiondoa katika ulimwengu wote; maana Bwana amenena hayo.
Katika siku hiyo watasema, Tazama, huyu ndiye Mungu wetu, Ndiye tuliyemngoja atusaidie; Huyu ndiye Bwana tuliyemngoja, Na tushangilie na kuufurahia wokovu wake.
Kwa maana mkono wa Bwana utatulia katika mlima huu.
Zab. 23:1-3,5-6
Bwana ndiye mchungaji wangu,
Sitapungukiwa na kitu.
Katika malisho ya majani mabichi hunilaza.
(K) Nitakaa nyumbani mwa Bwana milele.
Kando ya maji ya utulivu huniongoza,
Hunihuisha nafsi yangu na kuniongoza.
Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake.
(K) Nitakaa nyumbani mwa Bwana milele.
Waandaa meza mbele yangu,
Machoni pa watesi wangu.
Umenipaka mafuta kichwani pangu,
Na kikombe changu kinafurika.
(K) Nitakaa nyumbani mwa Bwana milele.
Hakika wema na fadhili zitanifuata,
Siku zote za maisha yangu;
Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele.
(K) Nitakaa nyumbani mwa Bwana milele.
Shangilio
Aleluya, aleluya,
Tazama Bwana atakuja kuwaokoa watu wake, Heri walio tayari kumlaki.
Aleluya.
Mt. 15:29-37
Siku ile: Yesu alifika kando ya bahari ya Galilaya; akapanda mlimani, akaketi huko. Wakamwendea makutano mengi wakimletea viwete, vipofu, mabubu, vilema, na wengine wengi, wakawaweka miguuni pake; akawaponya; hata ule mkutano wakastaajabu, walipowaona mabubu wanasema, vilema wanakuwa wazima, viwete wanakwenda, na vipofu wanaona; wakamtukuza Mungu wa Israeli.
Yesu akawaita wanafunzi wake, akasema, Nawahurumia mkutano, kwa kuwa yapata siku tatu wamekaa pamoja nami, wala hawana kitu cha kula; tena kuwaaga wakifunga sipendi, wasije wakazimia njiani. Wanafunzi wake wakamwambia, Tupate wapi mikate mingi hapa nyikani, hata kushibisha mkutano mkuu namna hii? Yesu akawaambia, Mnayo mikate mingapi? Wakasema, Saba, na visamaki vichache.
Akawaagiza mkutano waketi chini; akaitwaa ile mikate saba na vile visamaki, akashukuru akavimega, akawapa wanafunzi wake, nao wanafunzi wakawapa makutano. Wakala wote wakashiba; wakayaokota masazo ya vipande vya mikate, makanda saba, yamejaa.
Maoni
Ingia utoe maoni