Masomo ya Misa
Jumatano ya 34 ya Mwaka (Jumatano, Novemba 29, 2017)
Dan. 5:1-6,13-14.16-17,23-28
Belshaza, mfalme, aliwafanyia wakuu wake elfu karama kubwa, akanywa divai mbele ya elfu hao. Belshaza, alipokuwa akionja ile divai, akaamuru wavilete vile vyombo vya dhahabu na fedha, ambavyo baba yake, Nebukadreza, alivitoa katika hekalu lililokuwako Yerusalemu; ili kwamba mfalme, na wakuu wake, na wake zake, na Masuria wake, wapate kuvinywea. Basi wakavileta vile vyombo vya dhahabu, vilivyotolewa katika hekalu la nyumba ya Mungu lililokuwapo Yerusalemu; na mfalme, na wakuu wake, na wake zake, na Masuria wake, wakavinywea. Wakanya divai, wakaisifu miungu ya dhahabu, na ya fedha, na ya shaba, na ya chuma, na ya mti, na ya mwe. Saa iyo hiyo vikatokea vidole vya mkono wa mwanadamu, vikaandika katika chokaa ya ukuta wa nymba ya enzi ya mfalme, mahali palipokikabili kinara; naye mfalme akakiona kitanga cha ule mkono ulioandika. Ndipo uso wa mfalme ukambadilika; fikira zake zikamfadhaisha; viungo vya viuno vyake vikalegea; magoti yake yakagongana.
Ndipo Danieli akaletwa mbele ya mfalme. Na mfalme akanena, akamwambia Danieli, Je! Wewe ndiwe DAnieli yule, aliye mmoja wa wana wa Yuda waliohamishwa, ambao mfalme, baba yangu, aliwaleta huku toka Yerusalemu? Nimesikia habari zako, kwamba roho ya miungu imo ndani yako, na kwamba nuru na ufahamu na akili bora zimeonekana kwako. Nimesikia habari zako, kwamba waweza kuleta tafsiri, na kufumbua mafumbo; haya! Kama ukiweza kulisoma andiko hili, na kunijulisha tafsiri yake, utavikwa mavazi ya rangi ya zambarau, na kuwa na mkufu wa dhahabu shingoni mwako, nawe utakuwa mtu wa tatu katika ufalme.
Ndipo Danieli akajibu, akasema, mbele ya mfalme; Zawadi zako zishike wewe mwenyewe; na thawabu zako mpe mtu mwingine; walakini nitamsomea mfalme maandiko haya, na kumjulisha tafsiri yake. Basi umejiinua juu ya Bwana wa mbingu; nao wamevileta vyombo vya nyumba yake mbele yako; na wewe, na wakuu wako, na wake zako, na Masuria wako, mmevinywea; nawe umeisifu miungu ya fedha nay a dhahabu, na ya shaba, na ya chuma, na ya mti, na ya mawe; wasioona, wala kusikia, wala kujua neno lolote; na Mungu yule, ambaye pumzi yako I mkononi mwake, na njia zote ni zake, hukumtukuza. Ndipo kile kitanga cha ule mkono kikaletwa kutoka mbele zake, na maandiko haya yameandikwa.
Na maandiko yaliyoandikwa ni haya; Mene, Mene, Tekeli, na Peresi. Na tafsiri ya maneno haya ni hii; Mene, Mungu ameuhesabu ufalme wako na kuukomesha. Tekeli, umepimwa katika mizani nawe umeonekana kuwa umepunguka. Peresi, ufalme wako umegawanyika, nao wamepewa Wamedi na Waajemi.
Dan. 3:62-67
Jua na mwezi, mhimidini Bwana;
Msifuni na kumwadhimisha milele.
Nyota za mbinguni, mhimidini Bwana;
Msifuni na kumwadhimisha milele.
(K) Msifuni na kumwadhimisha Bwana milele.
Manyunyu yote na ukungu, mhimidini Bwana;
Msifuni na kumwadhimisha milele.
Pepo zote, mhimidini Bwana;
Msifuni na kumwadhimisha milele.
(K) Msifuni na kumwadhimisha Bwana milele.
Moto na hari, mhimidini Bwana;
Msifuni na kumwadhimisha milele.
Kipupwe na musimu, mhimidini Bwana;
Msifuni na kumwadhimisha milele.
(K) Msifuni na kumwadhimisha Bwana milele.
1Pet. 1:25
Aleluya, aleluya,
Neno la Bwana hudumu hata milele, na neno hilo ni neno lile jema lililohubiriwa kwenu.
Aleluya.
Lk. 21:12-19
Yesu aliwaambia wanafunzi wake; Watawakamata na kuwaudhi; watawapeleka mbele ya masinagogi, na kuwatia magerezani, mkipelekwa mbele ya wafalme na maliwali kwa ajili ya jina langu. Na hayo yatakuwa ushuhuda kwenu. Basi, kusudieni mioyoni mwenu, kutofikirifikiri kwanza mtakavyojibu; Kwa sababu mimi nitawapa kinywa na hekima ambayo watesi wenu wote hawataweza kushindana nayo wala kuipinga. Nanyi mtasalitiwa na wazazi wenu, na ndugu zenu, na jamaa zenu, na rafiki zenu, nao watawafisha baadhi yenu. Nanyi mtachukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu. Walakini hautapotea hata unywele mmoja wa vichwa vyenu. Nanyi kwa subira yenu mtaziponya nafsi zenu.
Maoni
Ingia utoe maoni