Masomo ya Misa
Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme (Jumapili, Novemba 26, 2017)
Eze. 34:11-12, 15-17
Bwana Mungu asema hivi; Tazama mimi mwenyewe, naam, mimi, nitawatafuta kondoo zangu, na kuwaulizia. Kama vile mchungaji atafutavyo kondoo zake, siku ile anapokuwa kati ya kondoo zake waliotawanyika; ndivyo nitakavyowatafuta kondoo zangu; nami nitawaokoa katika mahali pote walipotawanyika, katika siku ya mawingu na giza. Mimi mwenyewe nitawalisha kondoo zangu, nami nitawalaza, asema Bwana Mungu. Nami nitawatafuta waliopotea, nitawarudihsa waliofukuzwa, nitawafunga waliovunjika, nitawatia nguvu wagonjwa; nao wanono na wenye nguvu nitawaharibu; nitawalisha hukumu. Na kwa habari zenu, Enyi kundi langu, Bwana Mungu asema hivi; Tazama, nahukumu kati ya mnyama na mnyama, kondoo waume na mbuzi waume pia.
Zab. 23;1-3, 5-6
Bwana ndiye mchungaji wangu,
Sitapungukiwa na kitu,
Katika malisho ya majani mabichi hunilaza.
(K) Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu.
Kando ya maji ya utulivu huniongoza;
Huniuisha nafsi yangu, na kuniongoza,
Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake.
(K) Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu.
Waandaa meza mbele yangu,
Machoni pa watesi wangu.
Umenipaka mafuta kichwani pangu,
Na kikombe changu kinafurika.
Hakika wema na fadhili zitanifuata,
Siku zote za maisha yangu.
Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele.
(K) Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu.
1Kor. 15:20-26, 28
Kristo amefufuka katika wafu, limbuko lao waliolala. Maana kwa kuwa mauti ililetwa na mtu, kadhalika na kiyama ya wafu ililetwa na mtu. Kwa kuwa kama katika Adamu wote wanakufa, kadhalika katika Kristo wote watahuishwa. Lakini kila mmoja mahali pake, limbuko ni Kristo; baadaye walio wake Kristo, atakapokuja. Hapo ndipo mwisho, atakapompa Mungu Baba ufalme wake; atakapobatilisha utawala wote, na mamlaka yote, na nguvu. Maana sharti amiliki yeye, hata awaweke maadui wake wot echini ya miguu yake. Adui wa mwisho atakayebatilishwa ni mauti. Basi, vitu vyote vikiisha kutiishwa chini yake, ndipo Mwana mwenyewe naye atatiishwa chini yake yeye aliyemtiishia vitu vyote, ili kwamba Mungu awe yote katika wote.
Mk. 11:10
Aleluya, aleluya,
Abarikiwe Yeye ajaye kwa jina la Bwana: Ubarikiwe na Ufalme ujao, wa Baba yetu Daudi.
Aleluya.
Mt. 25:31-46
Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye, ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu wake; na mataifa yote watakusanyika mbele zake; naye atawabagua kama vile mchungaji abaguavyo kondoo na mbuzi; atawaweka kondoo mkono wake wa kuume, na mbuzi mkono wake wa kushoto. Kisha Mfalme atawaambia wale walioko mkono wake wa kuume, Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu; kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa na kiu, mkaninywesha; nalikuwa mgeni, mkanikaribisha; nalikuwa uchi, mkanivika; nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama; nalikuwa kifungoni, mkanijia. Ndipo wenye haki watakapomjibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona una njaa, tukakulisha, au una kiu tukakunywesha? Tena ni lini tulipokuona u mgeni, tukakukaribisha, au u uchi, tukakuvika? Ni lini tena tulipokuona u mgonjwa, au kifungoni, tukakujia? Na Mfalme atajibu, akiwaambia, Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi. Kisha atawaambia na wale walioko mkono wake wa kushoto, Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake; kwa maana nalikuwa na njaa, msinipe chakula; nalikuwa na kiu, msininyweshe; nalikuwa mgeni, msinikaribishe; nalikuwa uchi, msinivike; nalikuwa mgonjwa, na kifungoni, msije kunitazama. Ndipo hao pia watajibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona wewe una njaa, au una kiu, au u mgeni, au u uchi, au u mgonjwa, au u kifungoni, tusikuhudumie? Naye atawajibu, akisema, Amin, nawaambia, Kadiri msivyomtendea mmojawapo wa hao walio wadogo, hamkunitendea mimi. Na hao watakwenda zao kuingia katika adhabu ya milele; bali wenye haki watakwenda katika uzima wa milele.
Maoni
Ingia utoe maoni