Alhamisi. 19 Septemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumanne katika Oktava ya Pasaka (Jumanne, Machi 29, 2016)  

Somo la 1

Mdo 2:36-41

Basi nyumba yote ya Israeli na wajue yakini ya kwamba Mungu amemfanya Yesu huyo mliyemsulibisha kuwa Bwana na Kristo. Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu? Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu. Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie. Akawashuhudia kwa maneno mengine mengi sana na kuwaonya, akisema, Jiokoeni na kizazi hiki chenye ukaidi. Nao waliolipokea neno lake wakabatizwa; na siku ile wakaongezeka watu wapata elfu tatu.

Wimbo wa Katikati

Zab 33:4-5, 18-20, 22


Kwa kuwa neno la Bwana lina adili, Na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu.
Huzipenda haki na hukumu, Nchi imejaa fadhili za Bwana.
(K)Nchi imejaa fadhili za Bwana

Tazama, jicho la Bwana li kwao wamchao, Wazingojeao fadhili zake.
Yeye huwaponya nafsi zao na mauti, Na kuwahuisha wakati wa njaa.
(K)Nchi imejaa fadhili za Bwana

Nafsi zetu zinamngoja Bwana; Yeye ndiye msaada wetu na ngao yetu.
Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi, Kama vile tulivyokungoja Wewe.
(K)Nchi imejaa fadhili za Bwana

Injili

Yn 20:11-18

Lakini Mariamu alikuwa akisimama karibu na kaburi, nje yake, analia. Basi akilia hivi, aliinama na kuchungulia ndani ya kaburi. Akaona malaika wawili, wenye mavazi meupe, wameketi, mmoja kichwani na mmoja miguuni, hapo ulipolazwa mwili wake Yesu. Nao wakamwambia, Mama, unalilia nini? Akawaambia, Kwa sababu wamemwondoa Bwana wangu, wala mimi sijui walikomweka. Naye akiisha kusema hayo, akageuka nyuma, akamwona Yesu amesimama, asijue ya kuwa ni Yesu. Yesu akamwambia, Mama, unalilia nini? Unamtafuta nani? Naye, huku akidhania ya kuwa ni mtunza bustani, akamwambia, Bwana, ikiwa umemchukua wewe, uniambie ulipomweka, nami nitamwondoa. Yesu akamwambia, Mariamu. Yeye akageuka, akamwambia kwa Kiebrania, Raboni! (Yaani, Mwalimu wangu). Yesu akamwambia. Usinishike; kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini enenda kwa ndugu zangu ukawaambie, Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu. Mariamu Magdalene akaenda, akawapasha wanafunzi habari ya kwamba, Nimemwona Bwana, na ya kwamba amemwambia hayo.

Maoni


Ingia utoe maoni