Masomo ya Misa
Dominika ya 33 ya Mwaka (Jumapili, Novemba 19, 2017)
Mit. 31:10-13, 19-20, 30-31
Mke mwema, ni nani awezaye kumwona?
Maana kima chake chapita kima cha marijani.
Moyo wa mumewe humwamini, Wala hatakosa kupata mapato.
Humtendea mema wala si mabaya, siku zote za maisha yake.
Hutafuta sufu na kitani; taaa yake haizimiki usiku.
Hutia mikono yake katika kusokota; na mikono yake huishika pia.
Huwakunjulia maskini mikono yake;
Naam, huwanyoshea wahitaji mikono yake.
Upendeleo hudanganya, na uzuri ni ubatili; bali mwanamke amchaye Bwana, ndiye atakayesifiwa.
Mpe mapato ya mikono yake, na matendo yamsifu malangoni.
Zab. 128:1-5
Heri kila mtu amchaye Bwana,
Aendaye katika njia yake.
Heri yao wale wamchao Bwana,
Utakuwa mwenye heri na Baraka tele.
(K) Taabu ya mikono yako hakika utaila.
Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao,
Vyumbani mwa nyumba yako.
Wanao kama miche ya mizeituni,
Wakiizunguka meza yao.
(K) Taabu ya mikono yako hakika utaila.
Tazama, atabarikiwa hivyo, yule amchaye Bwana,
Bwana akubariki toka Sayuni,
Uone uheri wa Yerusalemu
Siku zote za maisha yako.
(K) Taabu ya mikono yako hakika utaila.
1The. 5:1-6
Ndugu zangu, kwa habari ya nyakati na majira, hamna haja niwaandikie. Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku. Wkati wasemapo. Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa. Bali ninyi, ndugu, hammo gizani, hata siku ile iwapate kama mwivi. Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa nuru, na wana wa mchana; sisi si wa usiku, wala wa giza. Basi tusilale usingizi kama wengine, bali tukeshe, na kuwa na kiasi.
Mt. 24:42, 44
Aleluya, aleluya,
Kesheni basin a kujiweka tayari, kwa maana hamjui saa atakayokuja, Mwana wa Adamu.
Aleluya.
Mt. 25:14 – 30
Ufalme wa mbinguni utafanana na mtu atakaye kusafiri, akawaita watumwa wake, akaweka kwao mali zake. Akampa mmoja talanta tano, na mmoja talanta mbili, na mmoja talanta moja; kila mtu kwa kadiri ya uwezo wake; akasafiri. Mara yule aliyepokea talanta tano akaenda, akafanya biashara nazo, akachuma faida talanta nyingine tano. Vile vile na yule mwenye mbili, yeye naye akachuma nyingine mbili faida. Lakini yule aliyepokea moja alikwenda akafukua chini, akaificha fedha ya bwana wake. Baada ya siku nyingi akaja bwana wa watumwa wale, akafanya hesabu nao. Akaja yule aliyepokea talanta tano, akaleta talanta nyingine tano, akisema, Bwana, uliweka kwangu talanta tano, tazama talanta nyingine tano nilizopata faida. Bwana wake akamwambia, Vema, mtumwa mwema na uaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako. Akaja na yule aliyepokea talanta mbili, akasema, Bwana, uliweka kwangu talanta mbili, tazama, talanta nyingine mbili nilizopata faida. Bwana wake akamwambia, Vema mtumwa mwema na uaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wakeo. Akaja na yule aliyepokea talanta moja, akasema, Bwana, nalitambua ya kuwa wewe u mtu mgumu, wavuna usipopanda, wakusanya usipotawanya; bali nikaogopa, nikaenda nikaificha talanta yako katika ardhi; tazama, unayo iliyo yako. Bwana wake akajibu, akamwambia, Wewe mtumwa mbaya na ulegevu, ulijua ya kuwa navuna nisipopanda, nakusanya nisipotawanya; basi, ilikupasa kuiweka fedha yangu kwa watoao riba; nami nikija ningalipata iliyo yangu na faida yake. Basi mnyang’anyeni talanta hiyo, mpeni yule aliye nazo talanta kumi. Kwa maana kila mwenye kitu atapewa, na kuongezewa tele, lakini asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa. Na mtumwa yule asiyefaa, mtupeni mbali katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.
Maoni
Ingia utoe maoni