Alhamisi. 19 Septemba. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya Pasaka (Jumapili, Machi 27, 2016)  

Somo la 1

Mdo 10:34, 37-43

Petro akafumbua kinywa chake, akasema, Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo; jambo lile ninyi mmelijua, lililoenea katika Uyahudi wote likianzia Galilaya, baada ya ubatizo aliouhubiri Yohana; habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye. Nasi tu mashahidi wa mambo yote aliyoyatenda katika nchi ya Wayahudi na katika Yerusalemu; ambaye walimwua wakamtundika mtini. Huyo Mungu alimfufua siku ya tatu, akamjalia kudhihirika, si kwa watu wote, bali kwa mashahidi waliokuwa wamekwisha kuchaguliwa na Mungu, ndio sisi, tuliokula na kunywa pamoja naye baada ya kufufuka kwake kutoka kwa wafu. Akatuagiza tuwahubiri watu na kushuhudia ya kuwa huyu ndiye aliyeamriwa na Mungu awe Mhukumu wa walio hai na wafu. Huyo manabii wote humshuhudia, ya kwamba kwa jina lake kila amwaminiye atapata ondoleo la dhambi.

Wimbo wa Katikati

Zab 118:1-2, 16-17, 22-23


Aleluya. Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele.
Israeli na aseme sasa, Ya kwamba fadhili zake ni za milele.
(K)Siku hii ndio aliyoifanya Bwana, Tutashangilia na kuifurahia.

Mkono wa kuume wa Bwana umetukuzwa; Mkono wa kuume wa Bwana hutenda makuu.
Sitakufa bali nitaishi, Nami nitayasimulia matendo ya Bwana.
(K)Siku hii ndio aliyoifanya Bwana, Tutashangilia na kuifurahia.

Jiwe walilolikataa waashi Limekuwa jiwe kuu la pembeni.
Neno hili limetoka kwa Bwana, Nalo ni ajabu machoni petu.
(K)Siku hii ndio aliyoifanya Bwana, Tutashangilia na kuifurahia.

Somo la 2

Kol 3:1-4

Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu.Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi. Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu. Kristo atakapofunuliwa, aliye uhai wetu, ndipo na ninyi mtafunuliwa pamoja naye katika utukufu.

Injili

Yn 20:1-9

Hata siku ya kwanza ya juma Mariamu Magdalene alikwenda kaburini alfajiri, kungali giza bado; akaliona lile jiwe limeondolewa kaburini. Basi akaenda mbio, akafika kwa Simoni Petro na kwa yule mwanafunzi mwingine ambaye Yesu alimpenda, akawaambia, Wamemwondoa Bwana kaburini, wala hatujui walikomweka. Basi Petro akatoka, na yule mwanafunzi mwingine, wakashika njia kwenda kaburini. Wakaenda mbio wote wawili; na yule mwanafunzi mwingine akaenda mbio upesi kuliko Petro, akawa wa kwanza kufika kaburini. Akainama na kuchungulia, akaona vitambaa vya sanda vimelala; lakini hakuingia. Basi akaja na Simoni Petro, akaingia ndani ya kaburi; akavitazama vitambaa vilivyolala, na ile leso iliyokuwako kichwani pake; haikulala pamoja na vitambaa, bali imezongwa-zongwa mbali mahali pa peke yake. Basi ndipo alipoingia naye yule mwanafunzi mwingine aliyekuwa wa kwanza wa kufika kaburini, akaona na kuamini. Kwa maana hawajalifahamu bado andiko, ya kwamba imempasa kufufuka.

Maoni


Ingia utoe maoni