Masomo ya Misa
Kumbukumbu ya Marehemu wote (Alhamisi, Novemba 02, 2017)
Hek 3:1-9
Roho zao wenye haki wamo mkononi mwa Mungu, wala maumivu hayatawagusa. Machoni pa watu walio wajinga walionekana kwamba wamekufa, na kufariki kwao kulidhaniwa kuwa ni hasara yao, na kusafiri kwao kutoka kwetu kuwa ni uharibifu wao; bali wao wenyewe wamo katika amani. Kwa sababu hata ikiwa (waonavyo watu) wanaadhibiwa, hata hivyo taraja lao limejaa kutokufa, na wakiisha kustahimili kurudiwa kidogo watapokea wingi wa mema. Kwa kuwa Mungu amewajaribu,na kuona kuwa wamestahili, kama dhahabu katika tanuru aliwajaribu, akawakubali mithili ya kafara. Wakati wa kujiliwa kwao kutang'aa, na kama vimulimuli katika mabua makavu watametameta. Watahukumu mataifa na kuwatawala kabila za watu; naye Bwana atawamiliki milele na milele. Wenye kumtumaini watafahamu yaliyo kweli, na waaminifu watakaa naye katika upendo; mradi neema na rehema zina wateule wake.
Zab 27:1-4,7-9,13-14
Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu, Nimwogope nani?
Bwana ni ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani?
Watenda mabaya waliponikaribia, Wanile nyama yangu,
Watesi wangu na adui zangu, Walijikwaa wakaanguka.
(K) Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu.
Jeshi lijapojipanga kupigana nami, Moyo wangu hautaogopa.
Vita vijaponitokea, Hata hapo nitatumaini.
Neno Moja nimelitaka kwa Bwana, Nalo ndilo nitakalolitafuta,
(K) Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu.
Nikae nyumbani mwa Bwana Siku zote za maisha yangu,
Niutazame uzuri wa Bwana, Na kutafakari hekaluni mwake.
Ee Bwana, usikie, kwa sauti yangu ninalia, Unifadhili, unijibu.
(K) Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu.
Uliposema, Nitafuteni uso wangu, Moyo wangu umekuambia, Bwana, uso wako nitautafuta.
Usinifiche uso wako, Usijiepushe na mtumishi wako kwa hasira.
Umekuwa msaada wangu, usinitupe, Wala usiniache, Ee Mungu wa wokovu wangu.
(K) Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu.
Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana Katika nchi ya walio hai.
Umngoje Bwana, uwe hodari, Upige moyo konde, naam, umngoje Bwana.
(K) Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu.
Rum 6:3-9
Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake? Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima. Kwa maana kama mlivyounganika naye katika mfano wa mauti yake, kadhalika mtaunganika kwa mfano wa kufufuka kwake; mkijua neno hili, ya kuwa utu wetu wa kale ulisulibishwa pamoja naye, ili mwili wa dhambi ubatilike, tusitumikie dhambi tena; kwa kuwa yeye aliyekufa amehesabiwa haki mbali na dhambi. Lakini tukiwa tulikufa pamoja na Kristo, twaamini ya kuwa tutaishi pamoja naye; tukijua ya kuwa Kristo akiisha kufufuka katika wafu hafi tena, wala mauti haimtawali tena.
Ufu. 14:13
Aleluya, aleluya,
Heri wafu wafao katika Bwana tangu sasa! Wapate kupumzika baada ya taabu zao, kwa kuwa matendo yao yafuatana nao.
Aleluya.
Mt 25:31-46
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye, ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu wake; na mataifa yote watakusanyika mbele zake; naye atawabagua kama vile mchungaji abaguavyo kondoo na mbuzi; atawaweka kondoo mkono wake wa kuume, na mbuzi mkono wake wa kushoto. Kisha Mfalme atawaambia wale walioko mkono wake wa kuume, Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu; kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa na kiu, mkaninywesha; nalikuwa mgeni, mkanikaribisha; nalikuwa uchi, mkanivika nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama; nalikuwa kifungoni, mkanijia. Ndipo wenye haki watakapomjibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona una njaa, tukakulisha, au una kiu tukakunywesha? Tena ni lini tulipokuona u mgeni, tukakukaribisha, au u uchi, tukakuvika? Ni lini tena tulipokuona u mgonjwa, au kifungoni, tukakujia? Na Mfalme atajibu, akiwaambia, Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi. Kisha atawaambia na wale walioko mkono wake wa kushoto, Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake; kwa maana nalikuwa na njaa, msinipe chakula; nalikuwa na kiu, msininyweshe; nalikuwa mgeni, msinikaribishe; nalikuwa uchi, msinivike; nalikuwa mgonjwa, na kifungoni, msije kunitazama. Ndipo hao pia watajibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona wewe una njaa, au una kiu, au u mgeni, au u uchi, au u mgonjwa, au u kifungoni, tusikuhudumie? Naye atawajibu, akisema, Amin, nawaambia, Kadiri msivyomtendea mmojawapo wa hao walio wadogo, hamkunitendea mimi. Na hao watakwenda zao kuingia katika adhabu ya milele; bali wenye haki watakwenda katika uzima wa milele.
Maoni
Ingia utoe maoni