Masomo ya Misa
Dominika ya 28 ya Mwaka (Jumapili, Oktoba 15, 2017)
Isa 25:6-10
Katika mlima huu Bwana wa majeshi atawafanyia mataifa yote karamu ya vitu vinono, karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wake, karamu ya vinono vilivyojaa mafuta, karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wake, iliyochujwa sana. Naye katika mlima huu atauharibu uso wa sitara iliyowekwa juu ya watu wote, na utaji ule uliotandwa juu ya mataifa yote. Amemeza mauti hata milele; na Bwana MUNGU atafuta machozi katika nyuso zote; na aibu ya watu wake ataiondoa katika ulimwengu wote; maana Bwana amenena hayo. Katika siku hiyo watasema, Tazama, huyu ndiye Mungu wetu, Ndiye tuliyemngoja atusaidie; Huyu ndiye Bwana tuliyemngoja, Na tushangilie na kuufurahia wokovu wake. Kwa maana mkono wa Bwana utatulia katika mlima huu.
Zab 23
Bwana ndiye mchungaji wangu,
Sitapungukiwa na kitu.
Katika malisho ya majani mabichi hunilaza,
Kando ya maji ya utulivu huniongoza.
Hunihuisha nafsi yangu;
(K) Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele
Huniongoza Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake.
Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti,
Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami,
Gongo lako na fimbo yako vyanifariji.
(K) Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele
Waandaa meza mbele yangu,
Machoni pa watesi wangu.
Umenipaka mafuta kichwani pangu,
Na kikombe changu kinafurika.
(K) Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele
Hakika wema na fadhili zitanifuata Siku zote za maisha yangu;
Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele.
(K) Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele
Flp 4:12-14, 19-20
Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; katika hali yo yote, na katika mambo yo yote, nimefundishwa kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa. Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu. Lakini mlifanya vema, mliposhiriki nami katika dhiki yangu. Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadiri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu. Sasa atukuzwe Mungu, Baba yetu, milele na milele. Amina.
Yn 14:6
Aleluya, aleluya
Mimi ndimi Njia, na Ukweli, na Uzima, asema Bwana; Mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi
Aleluya
Mt 22:1-14
Yesu alijibu, akawaambia tena kwa mithali, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyemfanyia mwanawe arusi. Akawatuma watumwa wake wawaite walioalikwa kuja arusini; nao wakakataa kuja. Akatuma tena watu kwa wengine, akisema, Waambieni wale walioalikwa, Tazameni, nimeandaa karamu yangu; ng'ombe zangu na vinono vimekwisha kuchinjwa, na vyote vimekuwa tayari, njoni arusini. Lakini hawakujali, wakaenda zao, mmoja shambani kwake, mmoja kwenye biashara yake; nao waliosalia wakawakamata watumwa wake, wakawatenda jeuri, na kuwaua. Basi yule mfalme akaghadhibika; akapeleka majeshi yake, akawaangamiza wauaji wale, akauteketeza mji wao. Kisha akawaambia watumwa wake, Arusi i tayari, lakini wale walioalikwa hawakustahili. Basi enendeni hata njia panda za barabara, na wote mwaonao waiteni arusini. Watumwa wale wakatoka wakaenda njia kuu, wakakusanya wote waliowaona, waovu kwa wema; arusi ikajaa wageni. Lakini alipoingia yule mfalme ili kuwatazama wageni wake, akaona mle mtu mmoja asiyevaa vazi la arusi. Akamwambia, Rafiki, uliingiaje humu nawe huna vazi la arusi? Naye akatekewa. Mfalme akawaambia watumishi, Mfungeni mikono na miguu, mchukueni mkamtupe katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Kwa maana waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache.
Maoni
Ingia utoe maoni