Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumamosi ya 27 ya Mwaka (Jumamosi, Oktoba 14, 2017)  

Somo la 1

Yoe. 3:12-21

Bwana asema hivi: Mataifa na wajihimize, wakapande juu katika bonde la Yehoshafati; maana huko ndiko nitakakoketi niwahukumu mataifa yote yaliyo pande zote. Haya! Utieni mundu, maana mavuno yameiva; njoni, kanyageni; kwa maana shinikizo limejaa, mapipa nayo yanafurika; kwani uovu wao ni mwingi sana.

Makutano makubwa, makutano makubwa, wamo katika bonde la kukata maneno! Kwa maana siku ya Bwana I karibu, katika bonde la kukata maneno.

Jua na mwezi vimetiwa giza, na nyota zimeacha kuangaza. Naye Bwana atanguruma toka Sayuni, atatoa sauti yake toka Yerusalemu; na mbingu nan chi zitatetemeka; lakini Bwana atakuwa kimbilio la watu wake, na ngome ya wana wa Israeli. Hivyo ndivyo mtakavyojua ya kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu, kikaaye Sayuni, mlima wangu mtakatifu; ndipo Yerusalemu utakapokuwa mtakatifu, wala wageni hawatapita tena ndani yake kamwe.

Tena itakuwa siku ile, ya kwamba milima itadondoza divai tamu, na vilima vitatiririka maziwa, na vijito vyote vya Yuda vitatoa maji tele; na chemchemi itatokea katika nyumba ya Bwana, na kulinywesha bonde la Shitimu. Misri itakuwa ukiwa, na Edomu itakuwa jangwa tupu, kwa sababu ya dhuluma waliowatenda wana wa Yuda; kwa sababu wamemwaga damu isiyo na hatia katika nchi yao. Bali Yuda atadumu milele, na Yerusalemu tangu kizazi hata kizazi. Nami nitaitakasa damu yao ambayo sijaitakasa; kwa maana Bwana ndiye akaaye Sayuni.

Wimbo wa Katikati

Zab. 97:1-2.5-6.11-12

Bwana ametamalaki, nchi na ishangilie,

Visiwa vingi na vifurahi.

Mawingu na giza vyamzunguka,

Haki na hukumu ndio msingi wa kiti chake. 

(K) Enyi wenye haki, mfurahieni Bwana.


Milima iliyeyuka kama nta mbele za Bwana,

Mbele za Bwana wa dunia yote.

Mbingu zimetangaza haki yake,

Na watu wote wameuona utukufu wake. 

(K) Enyi wenye haki, mfurahieni Bwana.


Nuru imemzukia mwenye haki,

Na furaha wanyofu wa moyo.

Enyi wenye haki, mfurahieni Bwana,

Na kulishukuru jina lake takatifu. 

(K) Enyi wenye haki, mfurahieni Bwana.

Shangilio

Zab. 25:4,5

Aleluya, aleluya,
Ee Bwana, unijulishe njia zako, unifundishe mapito yako.
Aleluya.

Injili

Lk. 11:27-28

Ikawa, Yesu alipokuwa akisema, mwanamke mmoja katika mkutano alipaza sauti yake, akamwambia Heri tumbo lililokuzaa, na matiti uliyonyonya. Lakini yeye alisema, Afadhali, heri walisikiao neno la Mungu na kulishika.

Maoni


Ingia utoe maoni