Masomo ya Misa
Sherehe ya Mt. Mathayo Mtume na Mwinjili (Alhamisi, Septemba 21, 2017)
Efe. 4:1-7, 11-13
Kwahiyo nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa; kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo; na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani. Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu. Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja. Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote.
Lakini kila mmoja wenu alipewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo.
Naye alitoa wengine kuwa mitume; na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti; na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kipimo cha ukamilifu wa Kristo.
Zab. 19:1-4
Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu, na anga laitangaza kazi ya mikono yake.
(K) Sauti yako imeenea duniani mwote.
Mchana husemezana na mchana, usiku hutolea usiku maalifa.
(K) Sauti yako imeenea duniani mwote.
Hakuna lugha wala maneno, sauti yao haisikilikani.
(K) Sauti yako imeenea duniani mwote.
Sauti yako imeenea duniani mwote, na maneno yao hata miisho ya ulimwengu.
(K) Sauti yako imeenea duniani mwote.
Mt. 9: 9-13
Naye Yesu alipokuwa akipita kutoka huko aliona mtu ameketi forodhani, aitwaye Matayo, akamwambia, ''Nifuate." Akaondoka, akamfuata.
Ikawa alipoketi nyumbani ale chakula, tazama, watoza ushuru wengi na wenye dhambi walikuja wakaketi pamoja na Yesu na wanafunzi wake.
Mafalisayo walipoona, waliwaambia wanafunzi wake, ''Mbona mwalimu wenu anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi?" Naye aliposikia, aliwaambia, ''Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi. Lakini nendeni, mkajifunze maana yake maneno haya: Nataka rehema, wala si sadaka. Kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi."
Maoni
Ingia utoe maoni