Masomo ya Misa
Jumatatu ya 24 ya Mwaka (Jumatatu, Septemba 18, 2017)
1Tim. 2:1-8
Basi, kabla ya mambo yote, nataka dua, na sala, na maombezi, na shukrani, zifanyike kwa ajili ya watu wote; kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, tuishi maisha ya utulivu na amani, katika utauwa wote na ustahivu. Hili ni zuri, nalo lakubalika mbele za Mungu Mwokozi wetu, ambaye hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli. Kwa sababu, Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu, ambaye alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote, utakaoshuhudiwa kwa majira yake. Nami kwa ajili ya huo naliwekwa niwe mhubili na mtume - nasema kweli, sisemi uongo -, mwalimu wa Mataifa katika imani na kweli. Basi nataka wanaume wasalishe kila mahali, huku wakiinua mikono iliyotakata pasipo hasira wala majadiliano.
Zab. 28: 2, 7-9
Uisikie sauti ya dua yangu nikuombapo, nikipainulia patakatifu pako mikono yangu.
(K) Na ahimidiwe Bwana maana amesikia sauti yangu.
Bwana ni nguvu zangu na ngao yangu, moyo wangu umemtumaini, nami nimesaidiwa; basi moyo wangu unashangilia, na kwa wimbo wangu nitakushukuru.
(K) Na ahimidiwe Bwana maana amesikia sauti yangu.
Bwana ni nguvu za watu wake, naye ni ngome ya wokovu kwa masiya wake.
(K) Na ahimidiwe Bwana maana amesikia sauti yangu.
Uwaokoe watu wako, uubariki urithi wako, uwachunge, uwachunguze milele.
(K) Na ahimidiwe Bwana maana amesikia sauti yangu.
Yn. 3: 16
Aleluya, aleluya,
Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu,
hata akamtoa Mwanawe pekee,
ili kila mtu amwaminiye asipotee,
bali awe na uzima wa milele.
Aleluya.
Lk 7: 1-10
Alipokwisha kuyamaliza maneno yake yote masikioni mwa watu, aliingia Kapernaumu. Na mtumwa wake akida mmoja alikuwa hawezi, karibu na kufa; naye ni mtu aliye mpenda sana. Aliposikia habari za Yesu, alituma wazee wa Wayahudi kwake kumwomba aje amponye mtumwa wake. Nao walipofika kwa Yesu, walimsihi sana wakisema, '' Amesitahili huyu umtendee neno hili; maana, analipenda taifa letu, naye alitujengea sinagogi." Basi Yesu akaenda pamoja nao. Hata alipokuwa si mbali na nyumba yake, yule akida alituma rafiki kwake, akamwambia, ''Bwana , usijisumbue, maana mimi sistahili wewe uingie chini ya dari yangu; kwahiyo nilijiona sistahili mwenyewe kuja kwako; lakini sema neno tu, na mtumwa wangu atapona. Kwa maana mimi nami ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, mwenye askari chini yangu; nikimwambia huyu, 'Nenda; na huyu; 'Joo,' huja; na mtumwa wangu, 'Fanya hivi', hufanya. " Yesu alipo sikia hayo alimstaajabia, akaugeukia mkutano uliokuwa ukimfuata, akasema ''Nawaambia, hata katika Israel sijaona imani kubwa namna hii." Na wale waliotumwa waliporudi nyumbani, wakamkuta yule mtumwa ni mzima.
Maoni
Ingia utoe maoni