Masomo ya Misa
Dominika ya 24 ya Mwaka (Jumapili, Septemba 17, 2017)
YbS 27:30-28:1-7
Hasira na ghadhabu, haya pia ni machukuzo na aliye mwenye dhambi yatampata. Mwenye kujilipiza kisasi ataona kisasi kutoka kwa Bwana; hakika Yeye atamfungia dhambi zake. Umsamehe jirani yako dhara alilokufanyia, hivyo nawe utasamehewa dhambi zako wakati utakaposali. Mwanadamu humkasirikia mwanadamu, je! atatafuta kuponywa na Bwana? Hamrehemu mwanadamu aliye mwenzake, je! atalalamika kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe? Aliye mwili na damu tu huilisha hasira yake, je! ni nani atakayempatanisha yeye kwa makosa yake? Basi kumbuka mwisho wako, uuache uadui; kumbuka uozi na mauti , ujiepushe na kutenda dhambi. Kumbuka zile amri, usikasirike na jirani yako; nawe ulikumbuke agano lake Aliye juu, umwachilie ujinga wake.
Zab. 103:1-4, 9-12
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
Naam, vyote vilivyo ndani yangu
Vilihimidi jina lake takatifu.
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
Wala usizisahau fadhili zake zote.
(K) Bwana amejaa huruma na neema,
si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa fadhili.
Ndiye anayekusamehe maovu yako yote,
Akuponya magonjwa yako yote.
Akomboa uhai wako na kaburi,
Akutia taji ya fadhili na rehema.
(K) Bwana amejaa huruma na neema,
si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa fadhili.
Yeye hatateta siku zote,
Wala hatashika hasira yake milele.
Hatutendei kadiri ya hatia zetu,
Wala halipi kwa kadiri ya maovu yetu.
(K) Bwana amejaa huruma na neema,
si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa fadhili.
Maana vile mbingu zilivyoinuka juu ya nchi,
Kadiri ile ile rehema zake ni kuu kwa wamchao.
Kama mashariki ilivyo mbali ma magharibi,
Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi.
(K) Bwana amejaa huruma na neema,
si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa fadhili.
Rum. 14:7-9
Hakuna mtu miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake, wala hakuna afaye kwa nafsi yake. Kwa maana kama tukiishi, twaishi kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tu mali ya Bwana. Maana Kristo alikufa akawa hai tena kwa sababu hii, awamiliki waliokufa na walio hai pia.
Yn. 13:34
Aleluya, aleluya,
Amri mpya nawapa, asema Bwana,
mpendane, kama vile nilivyowapenda ninyi.
Aleluya.
Mt. 18:21-35
Petro alimwendea Yesu akamwambia, Bwana ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? hata mara saba? Yesu akamwambia, Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini. Kwa sababu hii ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyetaka kufanya hesabu na watumwa wake. Alipoanza kuifanya, aliletewa mtu mmoja awiwaye talanta elfu kumi. Naye alipokosa cha kulipa, bwana wake akaamuru auzwe, yeye na mkewe na watoto wake, na vitu vyote alivyo navyo, akalipwe ile deni. Basi yule mtumwa akaanguka, akamsujudia akisema, Bwana, nivumilie, nami nitakulipa yote pia. Bwana wa mtumwa yule akamhurumia, akamfungua, akamsamehe ile deni. Mtumwa yule akatoka, akamwona mmoja wa wajoli wake, aliyemwia dinari mia; akamkamata, akamshika koo, akisema, Nilipe uwiwacho. Basi mjoli wake akaanguka miguuni pake, akamsihi, akisema, Nivumilie, nami nitakulipa yote pia. Lakini hakutaka, akaenda, akamtupa kifungoni, hata atakapoilipa deni. Basi wajoli wake walipoyaona yaliyotendeka, walisikitika sana, wakaenda wakamweleza bwana wao yote yaliyotendeka. Ndipo bwana wake akamwita, akamwambia, Ewe mtumwa mwovu, nalikusamehe wewe deni ile yote, uliponisihi; nawe, je! haikukupasa kumrehemu mjoli wako, kama mimi nilivyokurehemu wewe? Bwana wake akaghadhibika, akampeleka kwa watesaji, hata atakapoilipa deni ile yote. Ndiyo na Baba yangu wa mbinguni atakavyowatenda ninyi, msiposamehe kwa mioyo yenu kila mtu ndugu yake.
Maoni
Ingia utoe maoni