Jumanne. 14 Mei. 2024

Masomo ya Misa

KUMBUKUMBU YA BIKIRA MARIA MTAKATIFU WA MATESO (Ijumaa, Septemba 15, 2017)  

Somo la 1

Ebr. 5:7 – 9

Kristo, siku hizo za mwili wake, alimtolea yule, awezaye kumwokoa na kumtoa katika mauti, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa wa jinsi alivyokuwa mcha Mungu; na, ingawa ni Mwana, alijifunza kutii kwa mates ohayo yaliyompata; naye alipokwisha kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu wa milele kwa watu wote wanaomtii.

Wimbo wa Katikati

Zab. 31:1 – 5, 14 – 15, 19

Nimekukimbilia Wewe, Bwana,
Nisiaibike mbele kwa haki yako uniponye.
Unitegee sikio lako, uniokoe hima.
(K) Uniokoe, Ee Bwana, kwa ajili ya fadhili yako.

Uwe kwangu mwamba wa nguvu,
Nyumba yenye maboma ya kuniokoa,
Ndiwe genge langu na ngome yangu,
Kwa ajili ya jina lako uniongoze, unichunge.
(K) Uniokoe, Ee Bwana, kwa ajili ya fadhili yako.

Utanitoa katika wavu walionitegea kwa siri,
Maana wewe ndiwe ngome yangu.
Mikononi mwako naiweka roho yangu,
Umenikomboa, Ee Bwana, Mungu wa kweli.
(K) Uniokoe, Ee Bwana, kwa ajili ya fadhili yako.

Lakini mimi nakutumaini Wewe, Bwana,
Nimesema, Wewe ndiwe Mungu wangu.
Nyakati zangu zimo mikononi mwako;
Uniponye na adui zangu, nao wanaonifuatia.
(K) Uniokoe, Ee Bwana, kwa ajili ya fadhili yako.

Jinsi zilivyo nyingi fadhili zako
Ulizowawekea wakuchao;
Ulizowatendea wakukimbiliao
Mbele ya wanadamu!
(K) Uniokoe, Ee Bwana, kwa ajili ya fadhili yako.

Shangilio

Shangilio

Aleluya, aleluya,
Bikira Maria anafurahi yeye ameshinda na kupata nishani ya ushahidi pasipo kufa, alipokuwa chini ya msalaba wa Bwana.
Aleluya.

Injili

Yn. 19:25 – 27

Penye msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mamaye, na umbu la mamaye, Mariamu wa Klopa, na Mariamu Magdalene. Basi Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake, Mama, tazama, mwanao. Kisha akamwambia yule mwanafunzi, Tazama, mama yako. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani mwake.

Maoni


Ingia utoe maoni