Jumanne. 14 Mei. 2024

Masomo ya Misa

Jumatatu ya 23 ya Mwaka (Jumatatu, Septemba 11, 2017)  

Somo la 1

Kol. 1:24 – 2:3

Nayafurahia mateso niliyonayo kwa ajili yenu; tena nayatimiza katika mwili wangu yale yaliyopungua ya mateso ya Kristo, kwa ajili ya mwili wake, yaani kanisa lake; ambalo nimefanywa mhudumu wake, sawasawa na uwakili wa Mungu, niliopewa kwa faida yenu, nilitimize neno la Mungu; siri ile iliyofichwa tangu zamani zote na tangu vizazi vyote, bali sasa imefunuliwa kwa wtakatifu wake; ambao Mungu alipenda kuwajulisha jinsi ulivyo utajiri wa utukufu wa siri hii katika Mataifa, nao ni Kristo ndani yenu, tumaini la utukufu; ambaye sisi tunamhubiri habari zake, tukimwonya kila mtu, na kumfundisha kila mtu, katika hekima yote, tupate kumleta kila mtu mtimilifu katika Krito. Nami najitaabisha kwa neno lilo hilo, nikijitahidi kwa kadiri ya kutenda kazi kwake atendaye kazi ndani yangu kwa nguvu. Maana nataka ninyi mje jinsi ilivyo kuu juhudi yangu niliyo nayo kwa ajili yenu, na kwa ajili ya wale wa Laodikia, na wale wasioniona uso wangu katika mwili; ili wafarijiwe mioyo yao, wakiunganishwa katika upendo, wakapate utajiri wote wa kufahamu kwa hakika, wapate kujua kabisa siri ya Mungu, yaani, Kristo; ambaye ndani yake yeye hazina zote za hekima na maarifa zimesitirika.

Wimbo wa Katikati

Zab. 62:5-6, 8

Nafsi yangu, umngoje Mungu peke yake kwa kimya,
Tumaini langu hutoka kwake.
Yeye tu ndiye mwamba wangu na wokovu wangu,
Ngome yangu, sitatikisika sana.
(K) Kwa Mungu wokovu wangu na utukufu wangu.

Enyi watu, mtumainini siku zote,
Ifunueni mioyo yenu mbele zake;
Mungu ndiye kimbilio letu.
(K) Kwa Mungu wokovu wangu na utukufu wangu.

Shangilio

Zab 19:8

Aleluya, aleluya,
Amri ya Bwana ni safi,
huyatia macho nuru.
Aleluya.

Injili

Lk. 6:6-11

Ilikuwa siku ya sabato nyingine Yesu aliingia katika sinagogi akafundisha; na mlikuwamo mtu ambaye mkono wake wa kuume umepooza. Na waandishi na Mafarisayo walikuwa wakimvizia, ili waone kwamba ataponya siku ya sabato; kusudi wapate neno la kumshitakia. Lakini yeye atakayatambua mawazo yao, akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, Ondoka, simama katikati; akaondoka akasimama. Ndipo Yesu akawaambia, Nawauliza ninyi, Je! Ni halali siku ya sabato kutenda mema, au kutenda mabaya; kuponya roho au kuangamiza? Akawakazia macho wote pande zote, akamwambia yule mtu, Nyosha mkono wako. Akaunyosha; mkono wake ukawa mzima tena. Wakajawa na uchungu, wakashauriana wao kwa wao wamtendeje Yesu.

Maoni


Ingia utoe maoni