Jumatano. 08 Mei. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 22 ya Mwaka (Jumapili, Septemba 03, 2017)  

Somo la 1

Yer. 20:7-9

Ee Bwana, umenihadaa, nami nimehadaika; wewe una nguvu kuliko mimi, ukashinda; nimekuwa kitu cha kuchekesha, mchana kutwa; kila mtu hunidhihaki. Maana kila ninenapo napiga kelele; nalia, Dhuluma na uharibifu! Kwa kuwa neno la Bwana limefanywa shutumu kwangu, na dhihaka, mchana kutwa. Nami nikisema, Sitamtaja wala sitasema tena kwa jina lake; ndipo moyoni mwangu kumekuwamo kama moto uwakao, uliofungwa ndani ya mifupa yangu, nami nimechoka kwa kustahimili, wala siwezi kujizuia.

Wimbo wa Katikati

Zab. 63:1-5, 7-8

Ee Mungu, Mungu wangu, nitakutafuta mapema,
Nafsi yangu inakuonea kiu.
Mwili wangu wakuonea shauku,
Katika nchi kame na chovu, isiyo na maji.
(K) Ee Bwana, Mungu wangu, nafsi yangu inakuonea kiu.

Ndivyo nilivyokutazama katika patakatifu,
Nizione nguvu zako na utukufu wako.
Maana fadhili zako ni njema kuliko uhai,
Midomo yangu itakusifu.
(K) Ee Bwana, Mungu wangu, nafsi yangu inakuonea kiu.

Ndivyo nitakavyokubariki maadamu ni hai,
Kwa jina lako nitaiinua mikono yangu.
Nafsi yangu itakinai kama kushiba mafuta na vinono,
Kinywa changu kitakusifu kwa midomo ya furaha.
(K) Ee Bwana, Mungu wangu, nafsi yangu inakuonea kiu.

Maana Wewe umekuwa msaada wangu,
Na uvulini mwa mbawa zako nitashangilia.
Nafsi yangu imekuandama sana,
Mkono wako wa kuume unanitegemeza.
(K) Ee Bwana, Mungu wangu, nafsi yangu inakuonea kiu.

Somo la 2

Rum 12: 1-2

Basi ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana. Wala msifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.

Shangilio

Lk 21: 36

Aleluya, aleluya,
Kesheni kila wakati, ili mpate kuokoka,
na kusimama mbele ya Mwana wa Adamu.
Aleluya

Injili

Mt 16:21-27

Tangu wakati huo Yesu alianza kuwaonya wanafunzi wake ya kwamba imempasa kwenda Yerusalemu, na kupata mateso mengi kwa wazee na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na siku ya tatu kufufuka. Petro akamchukua, akaanza kumkemea, akisema. Hasha, Bwana, hayo hayatakupata. Akageuka, akamwambia Petro, nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu. Wakati huo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Mtu yeyote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayeipoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona. Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake? Kwa sababu Mwana wa Adamu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika zake; ndipo atakapomlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake.

Maoni


Ingia utoe maoni