Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Kumbukumbu ya Bikira Maria (Jumamosi, Agosti 05, 2017)  

Somo la 1

Wal. 25:1,8-17

Bwana alinena na Musa katika mlima wa Sinai, na kumwambia: Utajihesabia sabato za miaka, maana, miaka saba mara saba; zitakuwa ni siku za sabato saba za miaka kwenu, maana miaka arobaini na kenda. Ndipo utakapoipeleka pande zote hiyo baragumu yenye sauti kuu, siku ya kumi ya mwezi wa saba; katika siku hiyo ya upatanisho mtaipeleka baragumu katika nchi yenu yote. Na mwaka wa hamsini mtautakasa, na kupiga mbiu ya kuachwa mahuru katika nchi yote kwa watu wote waiketio; itakuwa ni yubile kwenu; nanyi kila mtu atairudia milki yake mwenyewe, nanyi mtarejea kila mtu kwa jamaa yake. Mwaka huo wa hamsini utakuwa ni yubile kwenu; msipande mbegu, wala msivune kitu hicho kimeacho chenyewe, wala msizitunde zabihu za mizabibu isiyopelewa. Kwa kuwa ni yubile; utakuwa mwaka mtakatifu kwenu; mtakula maongeo yake yatokayo shambani. Mwaka huo wa yubile mtairudia kila mtu milki yake. Tena kama ukimwuzia jirani yako chochote, au kununua chochote mkononi mwa jirani yako, msidanganyane wenyewe kwa wenyewe; kwa hesabu ya miaka iliyo baada ya yubile ndivyo utakavyonunua kwa jirani yako, na kama hesabu ya miaka ya mavuno ndivyo atakavyokuuzia wewe. Kama hesabu ya miaka ilivyo ni nyingi ndivyo utakavyoongeza bei yake, na kama hesabu ya miaka ilivyo ni chache ndivyo utakavyopunguza bei yake; kwani yeye akuuzia mavuno kama hesabu yake ilivyo. Wala msidanganyane; lakini utamcha Mungu wako; kwa kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.

Wimbo wa Katikati

Zab. 67:1-2, 4- 6-7

Mungu na atufadhili na kutubariki,
Na kutuangazia uso wake.
Njia yake ijulikane duniani,
Wokovu wake katikati ya mataifa yote.
(K) Watu na wakushukuru, Ee Mungu, Watu wote na wakushukuru.

Mataifa na washangilie,
Naam, waimbe kwa furaha,
Maana kwa haki utawahukumu watu,
Na kuwaongoza mataifa walioko duniani.
(K) Watu na wakushukuru, Ee Mungu, Watu wote na wakushukuru.

Nchi imetoa mazao yake;
Mungu, Mungu wetu, ametubariki.
Mungu atatubariki sisi;
Miisho yote ya dunia itamcha Yeye.
(K) Watu na wakushukuru, Ee Mungu, Watu wote na wakushukuru.

Shangilio

Zab. 25:4,5

Aleluya, aleluya,
Ee Bwana, unijulishe njia zako,
unifundishe mapito yako.
Aleluya.

Injili

Mt. 14:1 – 12

Mfalme Herode alisikia habari za Yesu, akawaambia watumishi wake, Huyo ndiye Yohane Mbatizaji; amefufuka katika wafu; na kwa hiyo nguvu hizo zinatenda kazi ndani yake. Maana Herode alikuwa amemkamata Yohane, akamfunga, akamtia gerezani, kwa ajili ya Herodia, mke wa Filipo nduguye. Kwa sababu Yohane alimwambia, Si halali kwako kuwa naye. Naye alipotaka kumwua, aliwaogopa watu, maana walimwona Yohane kuwa nabii. Hata ilipofika sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode, binti Herodia alicheza mbele ya watu, akampendeza Heorode. Hata akaahidi kwa kiapo ya kwamba atampa lolote atakaloliomba. Naye, huku akichochewa na mamaye, akasema, nipe hapa katika kombe kichwa cha Yohane Mbatizaji. Naye mfalme akasikitika; lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya wale walioketi chakulani pamoja naye, akaamuru apewe; akatuma mtu akamkata kichwa Yohane mle gerezani. Kichwa chake kikaletwa katika kombe, akapewa yule kijana; akakichukua kwa mamaye. Wanafunzi wake wakaenda, wakamchukua yule maiti, wakamzika; kisha wakaenda wakampasha Yesu habari.

Maoni


Ingia utoe maoni