Jumatatu. 13 Mei. 2024

Masomo ya Misa

Jumatano ya 17 ya Mwaka (Jumatano, Agosti 02, 2017)  

Somo la 1

Kut. 34 : 29-35

Hata ikawa, Musa aliposhuka katika mlima Sinai, na ztie mbao mbili za ushuhuda zilikuwa mkononi mwa Musa, hapo aliposhuka katika mlima, Musa hakujua ya kuwa ngozi ya uso wake iling’aa kwa sababu amesema na Bwana. Basi Haruni na wana wote wa Israeli walipomwona Musa, tazama, ngozi ya uso wake iling’aa; nao wakaogopa kumkaribia. Musa akawaita; Haruni na wakuu wote wa kusanyiko wakarudi kwake; Musa akasema nao. Baadaye wana wa Israeli wote wakakaribia; akawausia maneno yote ambayo Bwana amemwambia katika mlima Sinai. Na Musa alipokuwa amekwisha kusema nao, akatia utaji juu ya uso wake. Lakini desturi ya Musa ilikuwa alipoingia mbele za Bwana kusema naye, kuuvua huo utaji mpaka atoke; akatoka akawaambia wana wa Israeli maneno yote aliyoambiwa. Wana wa Israeli wakauona uso wa Musa ya kuwa ngozi ya uso wake Musa iling’aa; naye Musa akautia utaji juu ya uso wake tena, hata alipoingia kusema naye.

Wimbo wa Katikati

Zab. 99: 5-7, 9

Mtukuzeni Bwana, Mungu wetu,
sujuduni penye kiti cha miguu yake, ndiye mtakatifu.
(K) Bwana, Mungu wetu, ndiye mtakatifu.

Musa na Haruni miongoni mwa makuhani wake,
na Samweli miongoni mwao waliitiao jina lake,
walipomwita Bwana aliwaitikia.
(K) Bwana, Mungu wetu, ndiye mtakatifu.

Katika nguzo ya wingu alikuwa akisema nao.
Walishika shuhuda zake na amri aliyowapa.
(K) Bwana, Mungu wetu, ndiye mtakatifu.

Mtukuzeni Bwana, Mungu wetu,
sujuduni mkiukabili mlima wake mtakatifu,
maana Bwana, Mungu wetu, ndiye mtakatifu.
(K) Bwana, Mungu wetu, ndiye mtakatifu.

Shangilio

Yak 1:18

Aleluya, aleluya,
Kwa kupenda kwake mwenyewe, Baba alituzaa sisi kwa neno la kweli, tuwe kama limbuko la viumbe vyake.
Aleluya.

Injili

Mt. 13 :44-46

Yesu aliwaambia makutano mifano, Ufalme wa mbinguni umefanana na hazina iliyositirika katika shamba; ambayo mtu alipoiona, aliificha; na kwa furaha yake akaenda akauza alivyo navyo vyote, akalinunua shamba lile. Tena ufalme wa mbinguni umefanana na mfanya biashara, mwenye kutafuta lulu nzuri; naye alipoona lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda akauza alivyo navyo vyote, akainunua.

Maoni


Ingia utoe maoni