Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 17 ya Mwaka (Jumapili, Julai 30, 2017)  

Somo la 1

1 Fal. 3 : 5, 7-12

Huko Gibeoni Bwana alimtokea Sulemani katika ndoto ya usiku; Mungu akamwambia, Omba utakalo nikupe. Sulemani akasema, Ee Bwana, Mungu wangu, umenitawaza niwe mfalme mimi mtumwa wako badala ya Daudi baba yangu; nami ni mtoto mdogo tu; sijui jinsi inipasavyo kutoka wala kuingia. Na mtumwa wako yu katikati ya watu wako uliowachagua, watu wengi wasioweza kuhesabiwa, wala kufahamiwa idadi yao, kwa kuwa ni wengi. Kwa hiyo nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili niwahukumu watu wako, na kupambanua mema na mabaya; maana ni nani awezaye kuwahukumu hawa watu wako walio wengi? Neno hili likawa jema machoni pa Bwana, ya kuwa Sulemani ameomba neno hili. Mungu akamwambia, Kwa kuwa umeomba neno hili, wala hukujitakia maisha ya siku nyingi; wala hukutaka utajiri kwa nafsi yako; wala hukutaka roho za adui zako: bali umejitakia akili za kujua kuhukumu; basi, tazama, nimefanya kama ulivyosema. Tazama, nimekupa moyo wa hekima na wa akili; hata kabla yako hapakuwa na mtu kama wewe, wala baada yako hatainuka mtu kama wewe.

Wimbo wa Katikati

Zab. 118:57, 72, 76-77, 127-130

Bwana ndiye aliye fungu langu,
Nimesema kwamba nitayatii maneno yako.
Sheria ya kinywa chako ni njema kwangu,
Kuliko maelfu ya dhahabu na fedha.
(K) Sheria yako naipenda mno ajabu.

Nakuomba, fadhili zako ziwe faraja kwangu,
Sawasawa na ahadi yako kwa mtumishi wako.
Rehema zako zinijie nipate kuishi,
Maana sheria yako ni furaha yangu.
(K) Sheria yako naipenda mno ajabu.

Ndiyo maana nimeyapenda maagizo yako,
Kuliko dhahabu, naam, dhahabu iliyo safi.
Maana nayaona mausia yako yote kuwa ya adili,
Kila njia ya uongo naichukia.
(K) Sheria yako naipenda mno ajabu.

Shuhuda zako ni za ajabu,
Ndiyo maana roho yangu imezishika.
Kufafanusha maneno yako kwatia nuru,
Na kumfahamisha mjinga.
(K) Sheria yako naipenda mno ajabu.

Somo la 2

Rum 8 : 28-30

Twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwanawake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza.

Shangilio

Efe. 1 :17,18

Aleluya, aleluya,
Ewe Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Uyatie nuru macho ya mioyo yetu, Ili tujue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo.
Aleluya.

Injili

Mt. 13: 44-52

Yesu aliwaambia wafuasi wake: Ufalme wa mbinguni umefanana na hazina iliyositirika katika shamba; ambayo mtu alipoiona, aliificha; na kwa furaha yake akaenda akauza alivyo navyo vyote, akalinunua shamba lile. Tena ufalme wa mbinguni umefanana na mfanya biashara, mwenye kutafuta lulu nzuri; naye alipoona lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda akauza alivyo navyo vyote, akainunua. Tena ufalme wa mbinguni umefanana na juya, lilotupwa baharini, likakusanya wa kila namna; hata lilipojaa, walilivuta pwani; wakaketi, wakakusanya walio wema vyomboni, bali walio wabaya wakawatupa Ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia; malaika watatokea, watatenga waovu mbali na wenye haki, na kuwatupa katika tanuru ya moto; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Yesu aliwauliza, Mmeyafahamu hayo yote? Wakamwambia, Naam. Akawaambia, Kwa sababu hiyo, kila mwandishi mwenye elimu ya ufalme wa mbinguni amefanana na mtu mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale.

Maoni


Ingia utoe maoni