Jumatatu. 13 Mei. 2024

Masomo ya Misa

Kumbukumbu ya Mtakatifu Martha (Jumamosi, Julai 29, 2017)  

Somo la 1

Kut. 24:3-8

Musa aliwaambia watu maneno yote ya Bwana, na hukumu zake zote; watu wote wakajibu kwa sauti moja, wakasema, Maneno yote aliyoyanena Bwana tutayatenda. Basi Musa akayaandika maneno yote ya Bwana, akaondoka asubuhi na mapema, akajenga madhabahu chini ya mlima, na nguzo kumi na mbili, kwa hesabu ya kabila kumi na mbili za Israeli, akapeleka vijana wa wana wa Israeli, waliotoa sadaka za kuteketezwa, wakamchinjia Bwana sadaka za kuteketezwa, wakamchinjia Bwana sadaka za amani za ng’ombe. Musa akatwaa nusu ya ile damu, akaitia katika mabakuli; na nusu ya ile damu akainyunyiza juu ya madhabahu. Kisha akakitwaa kitabu cha agano akakisoma masikioni mwa watu; wakasema, hayo yote aliyoyanena Bwana tutayatenda, nasi tutatii. Musa akaitwaa ile damu, akawanyunyizia watu, akasema, hii ndiyo damu ya agano alilolifanya Bwana pamoja nanyi katika maneno haya yote.

Wimbo wa Katikati

Zab. 50:1-2, 5-6, 14-15

Mungu, Mungu Bwana, amenena, ameiita nchi,
Toka maawio ya jua hata machweo yake.
Tokea Sayuni, ukamilifu wa uzuri,
Mungu amemulika.
(K) Mtolee Mungu dhabihu za kushukuru.

Nikusanyieni wacha Mungu wangu,
Waliofanya agano nami kwa dhabihu.
Na mbingu zitatangaza haki yake,
Kwa maana Mungu ndiye aliye hakimu.
(K) Mtolee Mungu dhabihu za kushukuru.

Mtolee Mungu dhabihu za kushukuru;
Mtimizie Aliye juu nadhiri zako.
Ukaniite siku ya mateso;
Nitakuokoa, na wewe utanitukuza.
(K) Mtolee Mungu dhabihu za kushukuru.

Shangilio

Lk. 8:15

Aleluya, aleluya,
Wanabarikiwa wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao, hulisikia neno la Mungu na kulishika.
Aleluya.

Injili

Yn. 11:19-27

Watu wengi katika Wayahudi walikuwa wamekuja kwa Martha na Mariamu, ili kuwafariji kwa habari ya ndugu yao. Basi Martha aliposikia kwamba Yesu anakuja, alikwenda kumlaki; na Mariamu alikuwa akikaa nyumbani. Basi Martha akamwambia Yesu, Bwana, kama ungalikuwapo hapa, ndugu yangu hangalikufa. Lakini hata sasa najua ya kuwa yo yote utakayomwomba Mungu, Mungu atakupa. Yesu akamwambia, Ndugu yako atafufuka. Martha akamwambia, Najua ya kuwa atafufuka katika ufufuo siku ya mwisho. Yesu akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi; nave kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je! unayasadiki hayo? Akamwambia, Naam, Bwana, mimi nimesadiki ya kwamba wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, yule ajaye ulimwenguni.

Maoni


Ingia utoe maoni