Jumapili. 28 Aprili. 2024

Masomo ya Misa

Alhamisi ya 16 ya Mwaka (Alhamisi, Julai 27, 2017)  

Somo la 1

Kut. 19 :1-2, 9-11,16-20

Mwezi wa tatu baada ya kutoka Waisraeli katika nchi ya Misri, siku iyo hiyo wakafika jangwa la Sinai. Nao walipokuwa wameondoka Refidimu na kufika jangwa la Sinai, wakatua katika lile jangwa; Israeli wakapiga kambi huko wakiukabili mlima. Bwana akamwambia Musa, Tazama, mimi naja kwako katika wingu zito ili watu hawa wasikie nitakaposema nawe, nao wapate kukuamini wewe nawe hata milele. Musa akamwambia Bwana hayo maneno ya watu. Bwana akamwambia Musa, Enenda kwa watu hawa; ukawatakase leo na kesho: wakazifue nguo zao, wawe tavari kwa siku ya tatu; maana siku ya tatu Bwana atashuka katika mlima wa Sinai machoni pa watu hawa wote. Ikawa siku ya tatu, wakati wa asubuhi, palikuwa na ngurumo na umeme, na wingu zito juu ya mlima, na sauti ya baragumu iliyolia sana. Watu wote waliokuwa kituoni wakatetemeka. Musa akawatoa hao watu katika kituo, akawaltea ili waonane na Mungu; wakasimama pande za chini za kile kilima. Mlima wa Sinai wote pia ukatoa moshi, kwa sababu Bwana alishuka katika moto; na ule moshi wake ukapanda juu kama moshi wa tanuu, mlima wote ukatetemeka sana. Na hapo sauti ya baragumu ilipozidi kulia sana, Musa akanena, naye Mungu akamwitikia kwa sauti. Bwana akaushukia mlima, juu ya kilele cha mlima; Bwana akamwita Musa aende hata kilele cha mlima; Musa akapanda juu.

Wimbo wa Katikati

Dan. 3 : 52-56

Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.
Limehimidiwa jina lako takatifu, tukufu;
Lastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.
(K) Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.

Umehimidiwa katika hekalu la fahari yako takatifu;
Wastahili kusifika na kutukuzwa milele.
(K) Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.

Umehimidiwa juu ya kiti cha ufalme wako;
Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.
(K) Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.

Umehimidiwa utazamaye vilindi,
uketiye juu ya makerubi;
Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.
(K) Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.

Umehimidiwa katika anga la mbinguni
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.
(K) Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.

Shangilio

Zab. 130 : 5

Aleluya, aleluya,
Roho yangu inamngoja Bwana,
na neno lake nimeitumainia.
Aleluya.

Injili

Mt. 13 :10-17

Wanafunzi walimwambia Yesu, Kwa nini wasema nao kwa mifano? Akajibu, akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuzijua siri za ufalme wa mbinguni, bali wao hawakujaliwa. Kwa maana yeyote mwenye kitu atapewa, naye atazidishiwa tele; lakini yeyote asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa. Kwa sababu hii nasema nao kwa mifano; kwa kuwa wakitazama hawaoni, na wakisikia hawasikii, wala kuelewa. Na neno la nabii Isaya linatimia kwao, likisema: Kusikia mtasikia, wala hamtaelewa; kutazama mtatazama, wala hamtaona. Maana mioyo ya watu hawa imekuwa mizito, na kwa masikio yao hawasikii vema, na macho yao wameyafumba; wasije wakaona kwa macho yao, wakasikia kwa masikio yao, wakaelewa kwa mioyo yao, wakaongoka, nikawaponya. Lakini, heri macho yenu, kwa kuwa yanaona; na masikio yenu, kwa kuwa yanasikia. Kwa maana, amin, nawaambia: Manabii wengi na wenye haki walitamani kuyaona mnayoyaona ninyi, wasiyaone; na kuyasikia mnayoyasikia ninyi, wasiyasikie.

Maoni


Ingia utoe maoni