Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumanne ya 15 ya Mwaka (Jumanne, Julai 18, 2017)  

Somo la 1

Kut. 2 :1-15

Mtu mmoja wa nyumba ya Lawi aliondoka akaoa binti mmoja wa Lawi. Yule mwanamke akachukua mimba akazaa mwana, na alipoona ya kuwa ni mtoto mzuri akamficha miezi mitatu. Na alipokuwa hawezi kumficha tena, akampatia kisafina cha manyasi akakipaka sifa na lami, akamtia mtoto ndani yake, akakiweka katika majani kando ya mto. Umbu lake mtoto akasimama mbali ili ajue yatakayompata. Basi binti Farao akashuka, aoge mtoni, na vijakazi wake wakatembea kando ya mto; naye akakiona kile kisafina katika majani, akamtuma kijakazi wake kwenda kukileta. Akaifungua, akamwona mtoto, na tazama, mtoto yule analia. Basi akamhurumia, akasema, Huyu ni mmojawapo wa watoto wa Waebrania. Basi umbu lake mtoto akamwambia binti Farao, Je! niende nikamwite mlezi katika wanawake wa Kiebrania, aje kwako, akunyonyeshee mtoto huyu? Binti Farao akamwambia, Haya! enenda. Yule kijana akaenda akamwita mama yake yule mtoto. Binti Farao akamwambia, Mchukue mtoto huyu, ukaninyonyeshee, nami nitakupa mshahara wako. Yule mwanamke akamtwaa mtoto, akamnyonvesha. Mtoto akakua, naye akamleta kwa binti Farao, akawa mwanawe. Akamwita jina lake Musa, akasema, Ni kwa sababu nalimtoa majini. Hata siku zile, Musa alipokuwa mtu mzima, akatoka kuwaendea ndugu zake, akatazama mizigo yao. Akamwona Mmisri anampiga Mwebrania, mmojawapo wa ndugu zake. Basi akatazama huko na huko, na alipoona ya kuwa hapana mtu, akampiga Mmisri yule, akamficha ndani ya mchanga. Akatoka siku ya pili, na tazama, watu wawili wa Waebrania walikuwa wakipigana. Akamwambia yule aliyemdhulumu mwenzake. Mbona unampiga mwenzako? Yule akasema, Ni nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu wetu, na mwamuzi juu yetu? Je! wataka kuniua mimi kama ulivyomwua yule Mmisri? Musa akaogopa, akasema, Kumbe! jambo lile limejulikana. Basi Farao alipopata habari, akataka kumwua Musa; lakini Musa akakimbia mbele ya Farao, akakaa katika nchi ya Midiani; akaketi karibu na kisima.

Wimbo wa Katikati

Zab. 69 :3, 14, 30-31, 33-34

Uniponye kwa kunitoa matopeni,
Wala usiniache nikazama
Na niponywe nao wanaonichukia,
Na katika vilindi vya maji.
(K) Enyi mmtafutao Mungu,
mioyo yenu ihuishwe,
kwa kuwa Bwana huwasikia wahitaji.

Wakanipa uchungu kuwa chakula changu;
Nami nilipokuwa na kiu wakaninywesha siki.
Meza yao mbele yao na iwe mtego;
Naam, wakiwa salama na iwe tanzi.
(K) Enyi mmtafutao Mungu,
mioyo yenu ihuishwe,
kwa kuwa Bwana huwasikia wahitaji.

Nitalisifu jina la Mungu kwa wimbo,
Nami nitamtukuza kwa shukrani.
Nayo yatampendeza Bwana kuliko ng’ombe,
Au ndama mwenye pembe na kwato.
(K) Enyi mmtafutao Mungu,
mioyo yenu ihuishwe,
kwa kuwa Bwana huwasikia wahitaji.

Kwa kuwa Bwana huwasikia wahitaji,
Wala hawadharau wafunga wake.
Mbingu na nchi zimsifu,
Bahari na vyote viendavyo ndani yake.
(K) Enyi mmtafutao Mungu,
mioyo yenu ihuishwe,
kwa kuwa Bwana huwasikia wahitaji.

Shangilio

Zab. 119:18

Aleluya, aleluya,
Unifumbue macho yangu niyatazame,
maajabu yatokayo katika sheria yako.
Aleluya.

Injili

Mt. 11 :20-24

Yesu alianza kuikemea miji ile ambamo ndani yake ilifanyika miujiza yake iliyo mingi, kwa sababu haikutubu. Ole wako, Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni, wangalitubu zamani kwa kuvaa magunia na majivu. Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi Tiro na Sidoni kustahimili adhabu zao siku ya hukumu kuliko ninyi. Nawe Kapernaumu, je! utakuzwa mpaka mbinguni? utashushwa mpaka kuzimu; kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwako ingalifanyika katika Sodoma, ungalikuwapo mji huo hata leo. Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi nchi ya Sodoma kustahimili adhabu yake siku ya hukumu kuliko wewe.

Maoni


Ingia utoe maoni